Na Yohani Gwangway
“Demokrasia ni serikali ya watu, iliyochaguliwa na watu kwa ajili ya watu”. Ni maneno ya Rais wa 16 wa Marekani Abraham Lincoln mwaka 1863 akijaribu kutoa maana fupi ya demokrasia. Kwingineko demokrasia inaeleweka kuwa ni mfumo wa uongozi ambao huzingatia matakwa ya watu na maamuzi hufanyika kuzingatia maoni ya walio wengi bila kusahau maoni ya walio wachache.

Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika, inahesabiwa kama taifa lenye uongozi wa kidemokrasia katika mtazamo wa jumla. Tangu kupata uhuru kumekuwa na juhudi za kufikia viwango vya kidemokrasia ambavyo vinaendana na misingi ya ustaarabu wa watanzania. Wengine wamekuwa wakisema Afrika inahitaji kuwa na aina yake ya demokrasia ambayo inaendana na mazingira, tamaduni na mitazamo ya Afrika.
Historia ya bara la Afrika inaonesha mfumo wa utawala wa asili kama tawala za kifalme, kichifu na nyigine nyingi kabla ya ujio wa wakoloni. Baada ya kuja kwa wakoloni mambo mengi yalibadilika na mfumo wa kiutawala ulitoka katika mikono ya waafrika na kwenda katika mikono ya wakoloni.
Mifumo ya uongozi ya kikoloni ilikuwa ya kikandamizaji na kiunyonyaji hasa kwa watu wa Afrika. Wakoloni walihakikisha wanashika nyenzo zote za kiutawala ikiwemo njia kuu za uchumi. Aina hii ya uongozi iliwaumiza waafrika na baadaye kuanza kudai uhuru wao. Mfumo wa utawala uliokuwa unatumiwa na wakoloni haukutoka kwa watu, haukuwa wa kujali watu, na wala haukuwa ni kwa ajili ya watu.
Kutokana na aina hii ya utawala, mataifa ya Afrika na nchi nyingine ambazo zilitawaliwa kimabavu zikaanza kuhitaji mabadiliko ya mfumo wa uongozi. Mfumo ambao utakuwa unatokana na watu na uweze kuwajibishwa na watu.
Tanzania wakati wa ukoloni
Tanzania, wakati huo Tanganyika ilipita katika mikono ya wakoloni kadhaa. Kwa upande wa Tanganyika, tawala za Ujerumani na baadaye Uingereza zote zilikuwa na ubaguzi dhidi ya watu weusi. Ubaguzi huu ulikuwepo katika namna ya kuishi na namna ya kuongoza njia kuu za uchumi. Ujerumani ilianza kutawala Tanganyika baada ya mkutano wa Berlin mwaka 1885 ambao uliamua namna Afrika itakavyotawaliwa na wakoloni. Zanzibar kwa upande ilikuwa chini ya Ureno na baadaye chini nya utawala wa kisultan kutoka Muscat Oman
Baadaye mwaka 1916, wakati Vita vya Kwanza vya Dunia vikiwa vinaendelea, Uingereza iliichukua Tanganyika kutokana na kushindwa kwa Ujerumani na utawala wa Uingereza ulianza rasmi chini ya Gavana wake Sir Horace Byatt. Kutokana na ukweli kuwa tawala hizi zote hazikutokana na watu, hazipo kwa ajili ya watu ndiyo maana mabadiliko ya kudai uhuru yalianza.
Lengo likiwa ni kupata mfumo wa utawala wa watu (Watanganyika), unaotokana na watu na unaofanya kazi kwa ajili ya watu (Watanganyika).
Tanzania baada ya ukoloni
Baada ya harakati za muda mrefu chini ya Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) mwaka 1961, Tanzania (Tanganyika wakati huo) ilijipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza. Lakini bado kiu ikiwa ni kuwa mfumo wa utawala utakaotokana na wananchi kwa ajili ya wananchi. Kumekuwa na juhudi za hapa na pale katika kuimarisha mifumo hii ya uongozi kwa miaka kadhaa.

siku ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Picha: Bettmann/CORBIS.
Vuguvugu la kuachana na mfumo wa chama kimoja au utawala usioruhusu chaguzi zikaanza katika maeneo mengi. Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengi ilianza kubadilisha na kukubali baadhi ya mifumo ya utawala kutokana na mabadiliko na uhitaji. Ni kwa namna hii Tanzania ikaanza kuingia zama mpya zilizoleta siasa za ushindani.
Tanzania wakati wa mabadiliko wa vyama vingi 1992
Mwaka 1992, Tanzania iliingia rasmi katika mfumo wa vyama vingi baada ya mataifa kadhaa kushawishi aina hii ambayo itawezesha siasa za ushindani na uchaguzi kwa wananchi. Lengo likiwa ni kumpa mwananchi aamue ni aina gani ya uongozi anaouhitaji kutokana na sera mbalimbali za vyama vya siasa. Haikuwa rahisi kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Wananchi wengi walionesha kutamani kubaki na mfumo wa chama kimoja.
Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa mwaka 1991, ilikuwa na jumla ya wajumbe 23. Mwenyekiti alikuwa Jaji, Nyalali, Makamu mwenyekiti alikuwa ni Ndugu Abdulwahid Borafia huku katibu wa Tume akiwa ni Julius Sepeku.Wajumbe wengine 10 walitoka Tanzania Bara huku 10 wengine wakitoka Zanzibar.
Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza mambo mengi yaliyohusiana na mfumo wa utawala nchini Tanzania ikiwemo mabadiliko katika namna kuendesha siasa.
Baadaye viongozi wa nchi waliona ni vyema kuingia katika mfumo wa vyama vingi ili kuleta siasa za ushindani. Baadhi ya vyama vya siasa vikaanzishwa miaka ya 1992, 1993, 1994 na 1995 ambapo ulikuwa mwaka wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.
Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilifanya uchaguzi wake wa vyama vingi mwaka 1995 ukiwa na vyama 13. Katika uchaguzi huo uliokuwa wa ushindani, National Convention for Construction and Reform Party (NCCR-Mageuzi) ilikuwa na nguvu ya kukubalika ikiwa na mgombea wake Augustine Lyatonga Mrema. Ushindani huu ulikuwa kati yake na Benjamin William Mkapa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM). Katika nafasi ya Urais Benjamin William Mkapa alishinda uchaguzi huu kwa asilimia 61.8 huku Augustine Lyatonga Mrema akipata asilimia 27.8. Kuanzia hapo zikaanza siasa za ushindani. Vyama vikaanza kushindana kwa hoja na wananchi wakaanza kuwa na mbadala katika chaguzi zao.
Mwenendo na hali ya demokrasia sasa
Tangu kuanzishwa kwa mifumo mbalimbali ya kiutawala nchini Tanzania kumekuwa na hatua kubwa hadi miaka ya hivi karibuni. Siasa za Tanzania pamoja na namna ya kuongoza nchi zimetoa nafasi ya siasa za ushindani licha ya changamoto kadhaa. Kwa sababu taifa letu lilichagua kuwa la kidemokrasia, chaguzi nyingi hufanyika kupata viongozi wanaotokana na maamuzi ya wananchi.
Tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, chaguzi zingine za mwaka 2000, 2005, 2010,na 2015 zilitawaliwa na ushindani licha ya kuwepo kwa kasoro ndogo ndogo katika chaguzi hizi. Mwaka 2019 katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa 2020, kulitokea mabadiliko ambayo hayakuwahi kutarajiwa katika siasa za Tanzania.
Kulikuwa na matukio ya uenguaji wa wagombea hasa wa upinzani katika uchaguzi huo, wapinzani kushindwa kurudisha fomu kwa sababu ofisi zilifingwa na sababu zingine.
Matokeo yake, Chama tawala yaani CCM ilishinda uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 katika vijiji 12,260 sawa na asilimia 99.9, mitaa 4263 sawa na asilimia 100 na vitongoji 63,970 sawa na asilimia 99.4 huku kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ikishinda kwa asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa kwenye matokeo ya uchaguzi wa Rais.
Uchaguzi wa 2020, ndiyo ulioamsha hisia za wengi na kujiuliza kama Tanzania ni taifa linaloheshimu misingi ya demokrasia. Katika makala hii tumezungumza na wanasiasa, wachambuzi pamoja na wanasheria ili kupata mitazamo yao kuhusiana na hali ya demokrasia hapa nchini.
Licha ya matatizo mbalimbali baadhi ya wachambuzi wanasema hali ya demokrasia nchini bado ni nzuri. Hamduny Marcel ni mchambuzi wa siasa za Tanzania ambaye kwa mtazamo wake anaona mwelekeo ni mzuri
“Mwelekeo kwa ujumla ni mzuri kwa sababu demokrasia ina vipimo vyake. Demokrasia ni pamoja na uhuru wa kujieleza, demokrasia ni pamoja na hali ya watu kufanya uchaguzi kuchagua na kuchaguliwa, demokrasia ni pamoja na watu kuwa na usawa mbele ya sheria na vitu vingine vya namna hiyo.” Anasema Hamduny.
Uchaguzi katika miaka hii uligubikwa na mazingira mabaya kuanzia hatua ya kujaza fomu, kurudisha fomu, kampeni za wagombea, na matokeo yenyewe. Katika uchaguzi Mkuu wa 2020, chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichukua karibu viti vyote vya wabunge katika kile wapinzani waliita “Uchafuzi Mkuu” wa mwaka 2020.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliumizwa na wengine kupewa kesi kutokana na misimamo yao ya kisiasa. Jeraha hili katika taifa bado halijapona sawasawa kwani licha ya kufanyika juhudi za hapa na pale ikiwemo maridhiano kati ya chama tawala na vyama vya upinzani, lakini bado uwanja wa kidemokrasia ni kama umelalia upande mmoja.
Ni kwa sababu hizi Mweka hazina wa BAVICHA jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam, Elyneema Yuda anaona hali ya demokrasia nchini bado hairidhishi hasa akimulika masuala yanayoendelea ya kiusalama
“Hali ya Demokrasia nchini kwa kweli ninaweza kusema bado hairidhishi kwa kiwango kikubwa kwa sababu tunaona kuna ukiukwaji wa haki za binadamu tunaona watu wanapotea watu wanatekwa, lakini kiuhalisia kwenye nchi ya kidemokrasia usingetegemea haya yatokee.” Anaeleza Elyneema Yuda.
Kukiwa na doa katika mwenendo wa demokrasia Tanzania, Wakili Maduhu William ambaye ni Afisa wa Uchaguzi, Utawala na Demokrasia kutoka Kituo Cha Sheria Na Haki Za Binadamu (LHRC) anaona kuwa demokrasia nchini inategemea utashi wa viongozi waliopo kwa wakati husika.
“Demokrasia yetu imekuwa ikitegemea sana utashi wa Rais aliyepo madarakani kwa wakati huo kuliko mifumo ya kisera, kisheria na kikatiba. Maana yake ni kwamba akija Rais mzuri mwenye utashi mzuri wa kuheshimu haki za watu basi tutampongeza na kumsifia na kuona kwamba tuna ahueni. Akija Rais ambaye demokrasia kwake siyo kipaumbele tunaanza kulalamika kwa sababu nchi yetu haina mifumo thabiti.” Anasema Wakili Maduhu William.
Wakili Maduhu anashauri kuwa uwepo wa mifumo imara iliyo thabiti ndiyo mwarobaini wa desturi hii ya kuongoza wananchi kwa kutegemea maono na utashi wa viongozi.
“Kama taifa, hii tabia na desturi ya kutegemea maono, utashi wa mtu ni tabia ambayo tunapaswa kuiacha, tujenge mifumo. Tujenge taasisi imara ambazo zitamdhibiti yeyote hata kama akiwa nani. Wenzetu Wakenya mifumo yao ya kiuchaguzi na kitaasisi haingalii tamko la Rais, hata mahakama zao unaona mahakama inaweza ikafuta uchaguzi.” Anasema Wakili Maduhu.

Katika misingi ya demokrasia kuna mambo kadhaa ambayo taifa la kidemokrasia linahitaji kuyazingatia. Mambo haya ambayo mengi ni kuhusu mfumo wa uongozi ambayo angalau yanakubalika kwa walio wengi duniani. Katika sehemu hii tunamulika kama taifa letu linafuata misingi ya kidemokrasia au la.
Uhusika wa wananchi
Uhusika wa wananchi katika michakato ya kiuongozi ikiwemo haki yao ya kugombea, haki yao ya kupiga kura, haki yao ya kusikilizwa na nyinginezo ni msingi muhimu katika taifa la kidemokrasia. Mchakato huu unafanya wananchi kutambua kuwa ni wajibu wao kuamua hatma ya maisha yao. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kauli zinazoashiria kuwanyima nafasi ya kuchagua wamtakaye. Kauli hizi kwa nyakati tofauti zimeashiria kuwa kama wananchi hawatachagua chama tawala, basi hawataletewa maendeleo.
Rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli alishawahi kunukuliwa akisema kuwa hawezi kulipa mishahara na kuwapa magari wakurugenzi halafu wamtangaze mtu wa upinzani.
Kauli za aina hii zinaondoa uhusika wa wananchi katika kushiriki kuamua hatma ya viongozi wanaowataka kwa sababu kauli hizi ni ishara ya kutoheshimu maamuzi yao ya kumchagua mtu wamtakaye kwa kuwaletea hofu kuwa hawataletewa maendeleo.
Uchaguzi huru na wa haki
Chaguzi katika taifa la kidemokrasia zinatakiwa kuwa huru na haki. Uhuru huu unaanzia kuanzia mamlaka inayosimamia uchaguzi, mazingira ya uchaguzi, kuheshimu maamuzi ya wananchi, kutoingilia michakato ya uchaguzi kwa sababu za kisiasa na sababu zingine. Katika uchaguzi uliyopita nchini Tanzania, ambao waangalizi wa kimataifa walisema ni huru, mazingira yalionesha kuvunjwa kwa taratibu nyingi huku vyama vya upinzani vikisema hakukuwa na uchaguzi.

Baadhi ya matukio ya watu kutekwa yalitokea, wengine walipewa kesi za kisiasa, kulikuwa na matukio ya wazi ya kuingiza kura feki kwenye vituo na masuala mengine yaliyoashiria kutofuata misingi ya uchaguzi huru. Mfano mzuri ni tukio katika jimbo la Kawe ambapo aliyekuwa mgombea wa CHADEMA, Halima Mdee alikamata kura zilizokuwa zinaiingizwa kituoni hapo licha ya baadaye kutangazwa kwa Askofu Josephat Gwajima kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) kama mshindi.
Lakini siku za hivi karibuni kumeibuka kauli za baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakinadi kuwa mwaka 2020 serikali ndiyo ilitengeneza mazingira ya wao kushinda. Miongoni ni kauli ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Longido, Marco Ng’umbi.
“Sasa yale mazingira ya mwaka 2020 siyo kwamba yalikuja yenyewe kwa sababu nyinyi mlikuwa wagombea bora sana, ni mazingira ambayo yalikuwa yametengezwa na serikali na serikali ndiyo iliyoifanya kazi ile ya wewe kupita bila kupingwa.” Maneno ya Ng’umbi.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 2020, viongozi wa vyama vya upinzani waliitisha maandamano ambayo baadaye yalipelekea viongozi hao kuwa katika hali ya hatari kiusalama. Godbless Lema, Ezekiel Wenje, Tundu Lissu na wengine ambao siyo maarufu walikimbia nchi na kupata hifadhi ya muda nje ya nchi ili kuokoa maisha yao. Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe naye aliondoa biashara zake kutokana na kushambuliwa mara kwa mara. Ni katika mazingira haya, kama taifa tunahitaji kufanya tathmini ya kama kweli tunapiga hatua mbele au tunarudi nyuma kidemokrasia.
Licha ya matatizo haya wachambuzi wanaona bado kuna nafasi ya kuwa na uchaguzi huru na wa haki baada ya mabadiliko madogo yaliyofanyika na kuundwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)
“Suala la msingi la kuzingatia ni kwamba Tume hii tuliyonayo haijasimamia uchaguzi wowote, suala la msingi ni kusubiri na kuona Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi itakuwa sawa sawa na ile iliyokuwa Tume ya Uchaguzi na mitazamo yake na kadhalika! Na ikiwa hivyo basi liseme wakati huo siyo sasa.” Maoni ya Hamduny Marcel.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Taifa, John Pambalu anasema haoni mazingira ya uchaguzi huru na wa haki hasa akirejea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Chaguzi ambazo nimezishuhudia zile za mwaka 2020 na 2019 haziakisi kabisa kwamba taifa letu ni la kidemokrasia katika kipindi cha miaka minne, hata chaguzi ndogo zilizofanyika wakati wa utawala wa Rais Samia hauakisi kabisa maana ya demokrasia katika taifa letu.”Anasema Pambalu.
Licha ya juhudi za kubadilisha baadhi ya mambo bado kuna changamoto ya kauli za viongozi wakubwa ambazo zinaashiria kutoheshimu uchaguzi wa wananchi. Hivi karibuni kauli ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ilizua sintofahamu na baadaye kuondolewa katika nafasi yake.
Na kwa sababu mimi ni mjanja wa uchaguzi…Unajua matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye Box (sanduku), inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi, kuna halali, kuna nusu halali, na kuna haramu na zote zinaweza kutumika.” Kauli ya Nape Nnauye.
Utawala wa sheria
Kufuata utawala wa sheria ni hatua muhimu katika taifa linaloheshimu demokrasia na haki za watu. Dhana hii inasisitiza matumizi ya sheria zilizopo katika kufanya maamuzi pamoja na namna ya kuongoza watu. Hapa pia kama taifa tunahitaji kufanya tafakuri ya kina kama kweli tunaheshimu utawala wa sheria.
Kwa mfano, kuna matukio ya ukamataji yanayofanywa na Jeshi la Polisi kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali. Tukio la kukamatwa kwa Kombo Mbwana bila Jeshi la Polisi kukubali kumshikilia kwa siku 29 ni mfano halisi. Licha ya sheria kutaka maafisa wa Jeshi la Polisi kujitambulisha na kueleza kosa la mtuhumiwa, lakini katika baadhi ya matukio sheria hazifuatwi.

Masuala mengine ni kauli za viongozi ambazo zinaashiria kuchukua maamuzi ambayo hayafuati sheria zilizopo. Miongoni ni kauli ya Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila.
“Sioni faida ya kumpa nafasi mtu anayebomoa mlango na kuingia ndani na kuiba kitu hata kama ameiba chumvi. Uingiaji wake amekubali mambo matatu, kakubali kuiba, kakubali kuua, kakubali kuuawa. Na kama amekubali kuuawa, mnasubiri nini.” Anasema Chalamila.
Kuhusiana na kauli hii, Mchambuzi wa masuala ya siasa Hamduny anasema yeye anaona utawala wa sheria unafuatwa lakini tusifuate kauli za viongozi ambao nao wanatoa tu maoni yao.
“Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam siyo katiba ya Nchi, utawala wa sheria haujali nani, mahala gani, amezungumza nini. Ni Mkuu wa mkoa tu ambaye anaweza kutolewa na kuwekwa, kwa hiyo huyo hawezi kuwa mjadala katika suala kama hilo amezungumza maneno yaliyolingana na fikra zake.” Anasema Hamduny.
Uvumilivu wa kisiasa
Kuvumiliana kisiasa katika nchi yenye demokrasia ni afya. Uvumilivu huu ni pamoja na kuvumilia ukosoaji, kutovunjiana heshima, kujibu upande wa pili kwa hoja, kutohamasisha vurugu na kuhakikisha kuwa kauli zinazotolewa hazileti hasira na ghadabu kwa upande wa pili. Kutokana na umuhimu wa msingi huu, tunahitaji kujiuliza maswali kama tunapiga hatua au tunarudi nyuma.
Kuna kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ambazo zinaonesha kushindwa kuvumilia. Kauli ya Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kagera kusema kuwa wakosoaji wa Rais wasitafutwe wakipotezwa ni miongoni mwa mifano ya hivi karibuni.
“Kama kuna mtu anadhani anao uhuru wa kukaa mtandaoni na kisimu chake anashinda asubuhi kutwa nzima anatukana viongozi, Jeshi la Polisi hawa tukiwapoteza msiwatafute hawa, piga makofi kwa CCM”. Alisema Faris Buruhani, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kagera.
Ukiachana na hili kuna kauli ya aliyekuwa Katibu ya Itikadi na Uenezi wa CCM Paul Makonda, aliyedai Tanzania haina vyama vya upinzani.
“Tanzania haina chama cha upinzani, Tanzania ina watoa taarifa waliojikusanya kwa jina la upinzani.” Alisema Makonda.
Kauli za aina hii hazioneshi ukomavu na uvumilivu wa kisiasa. Maneno haya yanaweza kutafsiriwa kwa namna inayoonesha dharau na wakati mwingine kusababisha uvunjifu wa amani. Kwa upande wake John Pambalu anasema bado hakuna uvuilivu wa kisiasa akitolea mfano baadhi ya matukio.
“Hakuna uvumilivu wa kisiasa, pangekuwa na uvumilivu wa kisiasa tusingeshuhudia mauaji ya viongozi wa upinzani, tusingeshuhudia kupotezwa, kutekwa tusingeshuhudia dola ikiingilia kuharibu Siku ya Vijana Duniani na kukamata wafuasi wa CHADEMA zaidi ya 500.”
Mahakama huru
Miongoni mwa mihimili muhimu ya kiutawala ni pamoja na Mahakama. Ibara ya 107 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mamlaka yenye kauli ya mwisho kabisa ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni Mahakama. Ni kwa unyeti huu Mahakama inahitaji kuwa huru. Chombo hiki cha utoaji haki hakitakiwi kuyumbishwa na mhimili mwingine.

Nchini Tanzania kumekuwa na mazingira yanayozua maswali kuhusu uhuru wa Mahakama. Baadhi ya kauli za viongozi zinaonesha kutokubaliana na maamuzi ya mahakama katika mambo mengi. Lakini kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Rostam Aziz, mbunge wa zamani kupitia CCM kuwa mahakama zetu ni za kuelekezwa kwa simu inaonesha sintofahamu licha ya yeye mwenyewe kuomba msamaha juu ya matamshi hayo.
“Tunaona Mahakama zetu kwa nyakati tofauti tofauti zikilalamikiwa na baadhi ya wanasiasa na baadhi ya watu kwamba hazitendi haki.” Anasema Elyneema Yuda.
Uwazi na uwajibikaji
Dhana ya uwazi na uwajibikaji ni miongoni mwa msingi ya demokrasia ambayo inahitaji maamuzi yanayofanywa yawe wazi kwa wananchi ili kuwapa wananchi imani na serikali yao. Lakini pia pale maamuzi ya serikali au viongozi yatakapoonekana kuwa hayakuwa sahihi, basi ni lazima kutokee uwajibikaji. Kwa mfano, hatua ya uwajibikaji inafikiwa pale ambapo kiongozi anaona kuwa uzembe au makosa yake yamesababisha athari kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Hali ya uwajibikaji nchini Tanzania inasuasua. Kila mwaka ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) huibua madudu yanayoonesha matumizi yasiyofaa ya fedha za umma, uwizi au wakati mwingine rushwa lakini hakuna hatua inayochukuliwa. Mazingira haya katika taifa la kidemokrasia husababisha wananchi kuhisi wao hawana nafasi ya kusikilizwa na maovu yanayofanywa na viongozi hayawezi kutokomezwa.
“Uwazi na uwajibikaji bado ni shida kwenye mifumo yetu, mfano kwenye ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali zimeonesha kuna uwizi wa mali za umma , kuna ufisadi wa kutisha, lakini bado hawa watu hatujaona wakiwajibishwa.” Anasema Elyneema Yuda.
Katika dhana ya uwajibikaji kuna nyakati viongozi walitakiwa kujiuzulu lakini hawakufanya hivyo licha ya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Miongoni mwa kumbukumbu ni kujiuzulu kwa Waziri wa Mambo Ndani mwaka 1977, Ali Hassan Mwinyi kutokana na mauaji yaliyohusisha Jeshi la Polisi, lakini pia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowasa mwaka 2008 kutokana na sakata la Richmond.
Taifa letu ambalo linajivunia kuwa la kidemokrasia, linahitaji kuheshimu dhana ya uwazi pamoja na uwajibikaji katika mambo malimbali. Kitendo cha kushindwa kuwajibika ni tafsiri ya dharau kwa wananchi ambapo kwa Katiba ya Tanzania, mamlaka yote ya serikali yanatoka kwa wananchi.
Kuheshimu haki za binadamu
Kuzingatia utawala wa kidemokrasia ni pamoja na kuheshimu Haki za binadamu. Haki hizi ni zile ambazo mwanadamu anatakiwa kuzipata na hazitokani na mamlaka bali utu wa mtu. Katika baadhi ya matukio imeonekana kubugudhiwa kwa haki za watu kusema maoni yao, haki ya imani za watu na mambo mengine. Jeshi la Polisi limenyooshewa mkono mara kadhaa kutokana na kubambikiza watu kesi na wakati mwingine kuvunja haki za watuhumiwa.

Kuwepo kwa vitendo na matukio ya uvunjifu wa Haki za Binadamu kunamfikirisha Wakili Maduhu William kutoka LHRC na anaona kiza linapokuja suala la Haki za Binadamu nchini Tanzania.
“Kuna matukio ya watu kupotea na kutekwa, hivi karibuni kumekuwa na mwenendo wa haki za binadamu kuvunjwa…Bado wakuu wa mikoa kwa mfano wanatoa kauli za kamata weka ndani. Kwa hiyo haki za binadamu Tanzania bado ni kizungumkuti.” Wakili Maduhu.
Tanzania ikiwa ni nchi mwanachama wa mikataba mbalimbali ya kimataifa ya kulinda Haki za Binadamu kama vile Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (1948), Wakili Maduhu anashauri kama taifa tuheshimu maadhimio ya mikataba hiyo.
“Tunatokaje hapo, kwanza, ni kuheshimu maadhimio ambayo tumeadhimia kama nchi. Matamko mbalimbali ya kimataifa, mikataba ambayo tumeiingia ambayo inatoa maagizo mbalimbali kwa nchi wanachama kuheshimu, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu.” Anashauri Wakili Maduhu.
Uhuru wa maoni
Historia ya mwanadamu pamoja na asili yake, inaonesha mwanadamu ni kiumbe kinachohitaji kusikilizwa na kuheshimiwa maoni yake. Demokrasia inaheshimu asili hii na ni miongoni mwa vigezo vya kupima taifa linaloheshimu uongozi bora. Kwa hapa Tanzania uhuru wa maoni au watu kuongea uko katika ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania.
Hivi karibuni baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu walikamatwa kwa kutoa taarifa ya matukio ya kuvunjwa kwa haki za binadamu. Mfano mzuri ni sakata la Boniface Jacob na Godlisten Malisa waliotoa taarifa ya watu kupotea lakini kinyume chake waliambiwa wamefanya kosa la kusambaza taarifa za uongo. Hadi sasa kesi hii iko mahakamani.
Sakata jingine na la mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina ambaye pia alimkosoa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhusiana na ununuzi wa sukari nje ya nchi. Matokeo yake ni Mhe. Mpina kusimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge baada ya maamuzi ya Kamati ya maadili ya Bunge kumkuta na hatia ya kutoheshimu kiti cha Spika.
Matukio haya pamoja na mengine yanaonekana kunyamazisha uhuru wa wananchi kutoa maoni yao kuhusiana na mambo mbalimbali yanayohusu maisha yao. John Pambalu anasema haoni kama kuna uhuru wa watu kukosoa, bali kuna uhuru wa kusifia.
“Katika taifa letu tuna uhuru wa kuipongeza serikali, tuna uhuru wa kuisifia serikali. Ndiyo maana unaweza ukaona watu ambao katika siku za hivi karibuni ambao wamejizolea umaarufu sana ni wale wanaoipongeza serikali wanaitwa chawa wa mama wengine wanaitwa nyuki wa mama.”
Siku za hivi karibuni Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliwakana wanaojiita watoto wa mama pamoja na chawa wa mama akieleza kuwa kila mwananchi ni wa kwake. Licha ya kauli hii bado kuna watu wanaojiita chawa wa mama ambao kazi yao kubwa ni kusifia baadhi ya viongozi. Kusifia ni haki ya watu hawa lakini kinacholeta maswali ni pale ambapo ukosoaji unaonekana kuwa dhambi.
Kesho iliyo bora
Nchi yetu ambayo inasifika kwa utulivu na amani inahitaji kuzingatia misingi ya demokrasia katika kufanya maamuzi mbalimbali.
Mwenyekiti wa BAVICHA Taifa, John Pambalu anasema ili kuleta mafanikio katika demokrasia ya nchi yetu ni muhimu kupigania Katiba mpya
“Tuna kila sababu ya kupigania katiba mpya. Mabadiliko ya katiba ndiyo yatakayoleta uhuru wa mahakama, uhuru wa bunge na uhuru wa jambo lingine lolote.” Maneno ya John Pambalu.
Katika kuleta mageuzi ya mfumo wa uongozi, Tanzania kama ilivyo kwa mataifa mengine inatakiwa kuzingatia mambo kadha wa kadha.
Kwanza, wananchi wanatakiwa kufahamu wajibu wao na kushiriki ipasavyo katika shughuli za kisiasa. Wananchi wanatakiwa kuelimishwa kuwa ushiriki wao katika masuala ya nchi yao ni mwa msingi. Hakuna wananchi watakaoleta mabadiliko kama watanzania hawataamua kushiriki ipasavyo katika mambo yanayohusu kesho yao.
Pili, serikali na viongozi wa umma kwa ujumla wanatakiwa kufanya maamuzi yenye uwazi na yenye kuonesha uwajibikaji pale ambapo maamuzi hayo yamefanywa kwa uzembe na kuathiri masuala muhimu ya jamii. Viongozi mbalimbali pia wanatakiwa kuacha kutoa kauli zinazoashiria kutoheshimu wananchi hasa katika maamuzi yao ya uchaguzi.
Tatu, mahakimu na majaji wanatakiwa kufanya hukumu kwa kuzingatia haki. Kauli kuwa mwananchi atapoteza hela nyingi akienda mahakamani, zinatakiwa zisiwepo ili kuhakikisha kuwa kiwango cha uchumi wa mtu siyo kigezo cha kutoa hukumu. Mahakama zinatakiwa kujiheshimisha kwa kujinasua na malalamiko ya utendaji wa watu wake.
Nne, Bunge la Tanzania linatakiwa kuwakilisha wananchi ipasavyo na kujadili mambo yenye maslahi kwa umma. Bunge lisionekane kama chombo cha kulinda serikali, bali iwe na wajibu wa kuisimamia serikali ili kuleta mizania ya kiuongozi.
Kama kila raia atazingatia nafasi na mchango wake katika kuleta kesho iliyo bora, ni hakika tutajenga Tanzania tuitakayo ambayo kila mtu atafurahia matunda ya taifa letu.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


