Na Yohani Gwangway
Ashura ni mjasiriamali na mama wa watoto watatu ambaye anaishi katika Wilaya ya Nyamagani jijini Mwanza. Takriban miaka mitatu iliyopita Ashura alikuwa katika ndoa na mume wake wakiwa na furaha na amani. Lakini kwa sasa ndoa ya Ashura imevunjika baada ya ugomvi kati yake na mume wake uliotokana na kitendo cha ashura kukopa pesa kwa siri kutoka taasisi ndogo za fedha yaani Microfinance na baadaye kushindwa kulipa kutokana na riba kuwa kubwa hivyo deni kuongezeka.
Ni simulizi wa Mama wa makamo mwenye umri wa miaka 42 ambaye katika simulizi hii ataitwa Ashura ikiwa siyo jina lake halisi. Mama anayewakilisha kundi la Wajasirimali na wafanyabishara wengine wanaokutana na madhila baada ya kukutana na madeni makubwa yaliyotokana na riba kubwa wanazotozwa kutoka kwa taasisi ndogo za fedha nchini Tanzania.
Utoaji wa huduma za kifedha wa taasisi ndogo za fedha nchini Tanzania upo chini ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake (watoa huduma ndogo za kifedha wasiopokea amana). Katika baadhi ya mafunzo kuhusu elimu ya fedha ambayo yamekuwa yakitolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imekuwa ikieleza kuwa kiwango cha riba ambacho kitatozwa kwa waombaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi hizo ni asilimia 3.5 kwa mwezi.
Licha ya kiwango hiki cha Benki Kuu na sheria husika pamoja na kanuni zake kutoa miongozo wa utoaji wa huduma ndogo ndogo za fedha hasa kwenye upande wa riba kwa waombaji wa mikopo, lakini hali halisi inakinzana miongozo hiyo kwani taasisi hizo katika baadhi ya maeneo jijini Mwanza zimekuwa zikitoza riba kubwa ya asilimia 15, 20 hadi 40 kwa mwezi.
Kwa mfano, katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza mtu akikopeshwa shilingi 100,000 basi anatakiwa kurudisha kati ya shilingi 25,000 hadi 40,000 kwa mwezi jambo ambalo linamaanisha riba kati ya asilimia 25 hadi 40 kinyume na mwongozo wa benki kuu na kanuni za fedha. Kwa hiyo marejesho yake ya jumla kwa mwezi yanakuwa kati ya 125,000 hadi 140,000.

Mikopo inayotolewa na taasisi ndogo za fedha (Microfinaces) imewekwa katika kundi Daraja la pili la watoa huduma za fedha nchini Tanzania. Hadi mwaka 2024 mwezi Novemba kulikuwa na taasisi 2,221 watoa huduma za ndogo wa fedha wasiopokea amana zilizosajiliwa na BoT kote nchini Tanzania. Ukuaji wa taasisi hizi ni kupanua huduma kwa upande mmoja, lakini swali la msingi ni je, sheria na kanuni zinafuatwa na taasisi hizi katika kutoa mikopo?
Ashura ambaye ni mjasiriamali wa samaki, anasema aliwahi kuchukua mkopo kwenye taasisi moja ya fedha jijini Mwanza. Baada ya kuchukua mkopo huo Ashura alipata matatizo ya kifamilia jambo lililopelekea Ashura kutumia fedha hayo kwa matumizi ambayo hayakukusudiwa.
“Nilichukua shilingi milioni 2 nikiwa na lengo la kununua freezer ili kutunza samaki wasiharibike. Nilikuwa na uhakika kuwa nikiboresha biashara yangu itapanuka. Siku mbili baada ya kuchukua mkopo kulitokea tatizo kwetu ambapo mimi nilitakiwa kusaidia. Nilitumia zaidi ya shilingi milioni 1.5 ya mkopo. Hapo ndipo mambo yalipoanza kuharibika,” alisema Ashura.

Baada ya Ashura kutumia pesa hizi kwa matumizi mengine, biashara yake iliendelea kuyumba hadi ilipofika muda wa kurejesha. Licha ya kufahamu kuwa alichukua mkopo wa asilimia 40, Ashura hakuelewa kama mambo yanggebadilika na kulipa kiasi kikubwa cha pesa. Ilipofika mwisho wa mwezi, alitakiwa kulipa milioni 2.8 fedha ambayo hakuwa nayo.
“Baada ya mwezi walinipigia simu kuwa tarehe ya marejesho imefika. Nilikuwa sina pesa. Nikakubali kuwa niendelee kupewa mwezi mwingine. Na hapo pia sikuona mabadiliko makubwa ya deni langu na sikuwa na hofu ya kushindwa kulipa.”
Ashura alishindwa kulipa deni hili kwa miezi minne mfululizo jambo lililomfanya awe na deni la zaidi ya shilingi milioni 5.2. deni lilipofikia kiwango hiki Ashura hakuwa na namna ya kuendelea kumficha mume wake. Alimshirikisha mume wake ambaye hakuwa anafahamu haya. Mume wake alipokea taarifa hii kwa hasira na ugomvi ulizuka nyumani kwake. Hapo ndipo mwisho wa safari ya ndoa ya Ashura iliyodumu kwa zaidi ya miaka 10.
“Ilipopita miezi minne, nilitakiwa kulipa shilingi milioni 5.2. nilishtuka na nilijua sina uwezo wa kulipa bila msaada ya mume wangu. Nilipomshirikisha mume wangu, yeye alipata hasira kwa sababu alikuwa na hali mbaya kiuchumi. Deni hili lilikuwa kubwa kwetu. Mgogoro kati yetu ulianza. Ndoa yetu ikawa ya ugomvi hadi alipoamua kunitimua kwa kusema nafanya mambo kwa siri,” alifafanua Ashura.
Licha ya Ashura kumbembeleza mume wake ndoa yao ilifikia tamati mwaka 2023. Baadhi ya vitu vyao vya ndani vilichukuliwa ikiwemo Televisheni, Masofa, Kabati na vitu vingine vya thamani kama fidia ya deni hili. Kwa sasa Ashura ameanza maisha upya akiwa hana mtaji, ndoa yake ikiwa imevunjika huku baishara aliyokuwa anaifanya ikiwa imekufa.
“Mume wangu aliwaruhusu wachukue vitu vyetu ila alisema ndoa haiwezi tena kuendelea. Vitu vingi vilichukuliwa na mtaji wangu mdogo uliobaki nilimpa mume wangu ili awape wanaotudai. Sasa hivi hakuna kinachoeleweka na ninaona nimeanza maisha upya.”
Wafanyabiashara kama machinga, mamalishe, madereva bodaboda pamoja na makundi mengine wamekuwa wateja wakubwa wa mikopo hii mkoani Mwanza. Katika kata na mitaa ofisi za tasisi ndogo za fedha zimeongozeka na hivyo kurahisisha uchukuaji wa mikopo licha ya suala la riba kutozingatiwa.
Ukiachana na kisa cha Ashura, katika Wilaya ya Misungwi baadhi ya wachuuzi wa Samaki ni wahanga wa mikopo yenye riba kubwa. Maira Zabron ni mchuuzi wa Samaki ambaye huwa anatumia baiskeli kusambaza samaki. Maira alichukua mkopo wa shilingi 75,000 kutoka kwa taasisi moja ya kifedha katika eneo lake. Mkopo huu ulikuwa na riba ya asilimia 35. Maira ambaye haelewi suala la asilimia alishindwa kulipa mkopo wake kwa wakati. Taasisi hiyo ya kifedha ilimnyanganya baiskeli zake Maira kwa sababu aliandika baiskeli zake kama dhamana ya mkopo.
“Niliposhindwa kulipa kwa muda, walikuja kwangu wakanikuta. Sasa kwangu nilikuwa nimepaki baiskeli zangu nje baada ya mizunguko. Walichukua baiskeli mbiliwakaniambia watanirudishia nikilipa mkopo wote. Baadaye nilifanikiwa kulipa shilingi 80,000 na wakarudisha baiskeli moja. Nyingine walisema itakuwa ni mbadala wa kiasi kilichobaki,” alisema Maira, mchuuzi wa samaki.
Wamiliki wa taasisi ndogondogo za fedha wanatupiwa lawama na wakopaji kudai kuwa wanatumia uelewa wao mdogo kuwafilisi. Pia, baadhi ya kanuni za mikopo kama dhamana, mikataba pamoja na muda wa ziada wa kurudisha mikopo ukiwa hauzingatiwi. Kwa wanaochelewa kurudisha mikopo, baadhi ya vitu vyao huchukuliwa kwa nguvu.

Kwa Maira, kuchukuliwa baiskeli yake ya pili ambaye ilimuwezesha kuzunguka akiwa na msaidizi wake kumepunguza ufanisi katika kazi yake. Yeye anaona kuwa kutokuwa na uelewa kulimpoza licha ya kuhitaji fedha wakati anachukua mkopo.
“Wakati nachukua mambo hayakuwa magumu. Niliona nitamudu kulipa mkopo ndani ya muda. Walipochukua baiskeli yangu ya pili ambayo alikuwa anatumia msaidizi wangu, usambazaji wa Samaki umeshuka na kipato pia kimepungua,” Maira akieleza matokeo ya kushindwa kulipa mkopo kwa wakati.
Kutokana na kutosimamiwa ipasavyo kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 pamoja na Kanuni zake (watoa huduma ndogo za kifedha wasiopokea amana), badala ya kuwakwamua kiuchumi, mikopo hiyo hapa jijini Mwanza imepelekea baadhi ya wananchi hao kuwa wahanga kwa kufilisiwa mali zao, kudhalilishwa utu wao pamoja na kusababisha mafarakano ndani ya familia zao, na kujikuta wakizama kwenye dimbwi la umaskini.
Katika eneo la Nyahingi wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza, Amina ambaye ni mama wa mtoto mmoja alikimbia nyumba yake baada ya kudaiwa na taasisi moja ya mikopo iliyo katika kata ya Mkolani. Amina aliyekuwa amekopa shilingi milioni 1.8 alishindwa kulipa deni hilo jambo lilipelekea deni lake kufikia shilingi milioni 4.
Amina alikuwa akiishi mwenyewe katika nyumba yake na baada ya kushidwa kurejesha alitoroka kuepuka wanaomdai. Baada ya Amina kuondoka, maafisa waliotoka katika taasisi hiyo walifika kwake na kungoa madirisha ya Alluminiam huku wakiondoka na vitu vilivyo nje ya nyumba yake.
“Niliona usumbufu ulizidi nikaamua kuondoka ili niwatafutie hela yao. Baada ya kuondoka hajapita hata siku tatu, majirani walinipigia simu kuwa madirisha ya nyumba yako yamengolewa na maafisa wa taasisi iliyokuwa inanidai. Ilikuwa aibu kwa sababu watu wengine walikuwa hawajui kama nadaiwa. Walichukua madirisha na nje kulikuwa na banda la kuhamisha la kuku nalo walilibeba.” Maelezo ya Amina kuhusu mkopo aliouchukua.
Wamiliki wa taasisi ndogo za fedha waliozungumza kuhusiana na suala la kutoza riba kubwa, wameeleza kuwa riba ya asilimia 3.5 ambayo Wizara ya Fedha pamoja na BoT waliweka haina uhalisia. Mmiliki mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina wala taasisi yake amesema kuwa kama taasisi hizo zitafuata asilimia 3.5 kama BoT inavyotaka, basi ni wazi watashindwa kuendesha biashara yao na kufunga ofisi zao.
“Hakuna uhalisia wa riba na biashara tunayofanya. Wewe fikiria hiyo asilimia 3.5 unatakiwa ulipe kodi ya pango, unatakiwa ulipe wafanyakazi, gharama za umeme na hapohapo wewe upate faida. Ninadhani wakati Kanuni zinapitishwa hawakuangalia uhalisia. Nakumbuka tulifanya kikao na BoT nah ii hoja iliibuliwa” Alieleza Baraka ambaye ni mmiliki. Baraka siyo jina lake halisi.
Wamiliki hawa ambao wengi wao wanaelewa sheria na kanuni zilizopo, wanaonekana kutokubaliana na kiwango cha riba kilichowekwa kikanuni huku wakisisitiza kuwa inawaumiza wakopeshaji. Akizungumzia usimamizi wa kanuni Baraka amesema kuwa kanuni zilizopo zikisimamiwa, taasisi nyingi zinazokopesha zitafunga biashara.
“Kiwango hiki cha riba kikisimamiwa wengi tutafunga ofisi. BoT wenyewe wanajua kuwa hiki kiwango kinaumiza wakopeshaji na sisi tukifunga biashara yetu watakaoumia ni wananchi. Mabenki yana kanuni nguvu za kupata mkopo kuliko sisi. Hili jambo linahitaji busara” Baraka akielezea usimamizi wa kanuni.
Katika juhudi za kupata ufafanuzi kutoka kwa BoT ambayo ndiyo imepewa mamlaka ya kusimamia taasisi ndogo za fedha yaani Microfinance, BoT ilisema kuwa hakuna kanuni ya moja kwa moja inayotaka riba iwe asilimia 3.5. Maelezo haya ya BoT yanakuja ikiwa katika mafunzo mbalimbali waliyotoa kwa wadau wakisisitiza riba kuwa asilimia 3.5 kwa mwezi.
“Kutokana na mageuzi hayo, riba ya sasa inapangwa kutokana na soko(free market) kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine sifa alizonazo mkopaji (credit worthiness of a borrower), gharama za upatikanaji wa mtaji(cost of funds). Hivyo hakuna riba elekezi kwa mujibu wa sheria kma ilivyoainishwa katika swali la kwanza kuwa kuna riba ya asilimia 3.5”. Maelezo ya BoT wakijibu maswali ya Land Dwellers kuhusiana na kiwango cha riba.

Land Dwellers pia ilitafuta taarifa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo tovuti ya Wizara ya Fedha ambapo taarifa rasmi ya Wizara ya Fedha ilionesha kuwa taasisi ndogo za Fedha zinatakiwa kutoza riba ya asilimia 3.5 kwa mwezi na 42 kwa mwaka huku taarifa hii ikisisitiza kuwa yeyote anayekiuka kiwango hiki anavunja sheria.
Land Dwellers ilifanikiwa kuona baadhi ya mikataba ya wanaokopeshwa ambapo ilihakikisha kuwa katika taasisi zaidi ya 8 katika wilaya ya Nyamagana na Misungwi, taasisi za fedha zinachukua zaidi ya asilimia 3.5. kwa kiasi kikubwa baadhi ya wakopaji wanalipa asilimia 20 wengine 25, wengine 30 na kwa kiasi cha juu wengi wanatozwa asilimia 45. Pia Land Dwellers ilishuhudia wakopaji wakikatwa shilingi 5,000 katika mkopo wanaouchukua hii ikiitwa fedha ya fomu.
Kwa upande wa BoT imeeleza kuwa uwepo riba kubwa ya asilimia 25 hadi 40 kutoka taasisi ndogo za fedha vilevile huchangiwa pakubwa na baadhi ya taasisi hizo kutokuwa na leseni au vibali vya kutoa huduma hiyo, hivyo hutoa mianya ya kuendesha kazi zao bila kufuata sheria na kanuni za utoaji wa huduma.
“Hili hutokana na uwepo wa watoa huduma ndogo za fedha wanaofanya biashara bila kuwa na Ofisi, Leseni/kibali au kusajiliwa ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa hawaendeshi biashara zao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa. Vilevile kuwepo kwa watoa huduma wenye leseni ambao hutoa mikopo bila kuzingatiamatakwa ya sheria na Kanuni za usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha ikiwemo Kanuni za kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha,” imeeleza taarifa ya BoT.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


