Zitto: Nidhamu inahitajika kufikia shabaha ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

Na Zitto Kabwe

Leo inazinduliwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Shabaha ya Dira ni kuwa na Pato la Taifa la USD 1 trillion ambapo pato la mtu mmoja liwe wastani wa USD 7,000 kwa mwaka kutoka USD 1,200 za sasa. Hii maana yake ni kuwa Uchumi wetu (GDP) inapaswa kukua mara 13. Inawezekana, lakini katika Taifa lililo na mshikamano, lisilo na ubaguzi na lenye demokrasia. Msingi wa hayo ni HAKI. Kazi kubwa inapaswa kufanywa kwa NIDHAMU ya hali ya juu sana kufikia shabaha hiyo. Taifa lenye jamii ya uchawa uchawa haiwezi kuwa na nidhamu ya kufikia malengo tajwa.

Nidhamu ya kazi inahitajika kwa kila sekta

KILIMO: Kasi ya ukuaji wa Uchumi itapaswa kuongozwa na sekta ya Kilimo, kikue kwa kasi ya 8-10% kwa mwaka. Tunapaswa kuweka nguvu kubwa katika TIJA kwenye Kilimo, angalau tuongeze mavuno mara mbili (doubling) ya sasa katika kila Ekari ya mazao ya Kilimo. Nina mfano napenda kuutoa, wa zao la Pamba, ambapo ilhali mkulima wa Tanzania anapata kilo 250 – 300 kwa kila ekari ya Pamba, mkulima wa Benin anapata kilo 800 na mkulima wa Burkinafaso anapata kilo 1500. Hali ni mbaya zaidi kwenye Mahindi na Mpunga ambapo wakulima wetu wanapata gunia chache zaidi kutoka kila ekari 1!

Dira ya 2050 itafikiwa iwapo tutakuwa na nidhamu kwenye TIJA!

VIWANDA NA MADINI: Ni lazima tuongeze ajira kwa kuhakikisha mnyororo wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi unafungamanishwa na sekta yetu ya kilimo. Ni lazima kuongeza tija ya mazao yetu ili yasiuzwe yakiwa ghafi. Zamani niliwahi kuandika ningeanza na nini kati ya Reli ya SGR na Mgodi wetu wa Mchuchuma na Liganga. Ni jambo zuri tumejenga Reli ya SGR, lakini zaidi ya 75% ya fedha zilizotumika kwenye ujenzi huo zimekwenda nje ya nchi (Japan na Uturuki) kununua chuma na mataruma, ilhali chuma tunacho mchuchuma na Liganga Njombe na Ruvuma, mabehewa ya SGR yamekuja, lakini makochi na viti havijatengenezwa na mkonge wa Tanga wala Pamba ya Simiyu, ama ngozi ya mifugo yetu, tumeendelea kuuza ngozi ghafi, katani ghafi na pamba ghafi. Tuna hifadhi ya Dhahabu, Almasi na Shaba, na tuna Hifadhi ya Madini Adimu Duniani (Rare Earth Metals).

Dira ya 2050 itafikiwa iwapo tutakuwa na nidhamu katika usimamizi wa rasilimali madini na kuhakikisha sekta ya viwanda inaongeza thamani ya bidhaa za kilimo, madini na uvuvi.

AJIRA NA UMASIKINI: Watanzania wengi ni masikini na wengi wao wanazunguka kwenye mstari wa umasikini. Walio juu wakipata Dhoruba (shock) kidogo wanadondoka, walio chini wakipata Msukumo (boost) kidogo wanapanda. Wajibu wa Uongozi ni kuwapandisha walio chini na kuwahami walio juu wasidondoke. Hifadhi ya Jamii kwa wote ndio jawabu ya hilo. Njia nzuri ya kuongeza watu kwenye hifadhi ya Jamii ni kuongeza Ajira na Shughuli za maendeleo. Kwa sasa uchumi wetu hauzalishi Ajira za kutosha, vijana wengi hawana ajira kabisa, na hawana mitaji na mazingira wezeshi ya kujiajiri, hivyo tunaongeza tu watu wanaoanguka kwenye lindi la umasikini.

Dira ya 2050 itafikiwa iwapo kutakuwa na nidhamu katika kuhangaika  na masuala ya ajira na umasikini wa watu wetu.

HIFADHI YA JAMII NA MITAJI: Tanzania inahitaji kujenga uwezo wa ndani wa mitaji ili Sekta Binafsi ipate mitaji ya kuwekeza katika kukuza Uchumi. Uwezo wetu wa ndani wa kuweka akiba ni mdogo. Uwiano wa Akiba na Pato la Taifa (Savings – GDP ratio) ni chini ya 16%. Hivyo tunapaswa kujenga mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii (social security) ili kujenga uwezo wa watu wetu kuweka Akiba pamoja na kusaidia kuwatoa watu wetu kwenye umasikini. Uendeshaji wa miaka 25 sasa wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii una shida, Mafao na Vikokotoo havichochei watu kuweka akiba ya hifadhi ya jamii, mifuko yetu ya Bima ya Afya inakaribia kuanguka nk. Kwa nchi za wenzetu, mifuko ya Hifadhi ya Jamii ndio chanzo kikuu cha mitaji ya mikopo kwa Serikali na Sekta binafsi, huko kote tunakokopa nyingi ya fedha tunazokopeshwa zinatokana na akiba za hifadhi ya jamii, tunao wajibu wa kuhakikisha tunajenga akiba kubwa ya hifadhi ya jamii ili kuwa na uhakika wa mitaji ya ndani.

Dira ya 2050 itafikiwa iwapo kutakuwa na nidhamu katika kusimamia eneo hili la hifadhi ya jamii kwa wote.

JIOGRAFIA NA BANDARI: Jiografia yetu pekee inaweza kuifanya Nchi yetu kuwa na mapato ya kigeni ya zaidi ya USD 12 Bilioni kwa mwaka na makusanyo ya kodi ya USD 10 Bilioni kila mwaka kutoka katika Forodha (Customs) peke yake. Tumezungukwa na DRC, Zambia, Uganda, Rwanda, Burundi na Malawi ambao wanatutegemea sisi kuifikia bahari. Hivyo tuboreshe ufanisi wa Bandari ili utumike kusaidia sekta nyengine kama Usafirishaji, Biashara na Uhifadhi ili kuhakikisha Jiografia yetu inatufaidisha zaidi.

Dira ya 2050 itafikiwa iwapo tutakuwa na nidhamu katika matumizi na usimamizi wa bandari zetu.

UONGOZI NA SIASA: mwaka jana tumeona uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini, chama cha ANC kimeshindwa kupata kura za kutosha (majority) kwa mara ya kwanza tangu 1994, kitapaswa kuongoza na vyama vyengine, na inawezekana kabisa kisiwe kwenye uongozi miaka kadhaa mbele. Hapa kwetu CCM wanajiona wao tu ndio wenye haki ya kuongoza, hata pale wanapokataliwa kwa kura na wananchi, na vyombo vya Dola vimetumika kusaidia CCM kusalia madarakani hata pale walipokataliwa, tunayo mifano ya Zanzibar tangu 1995, mfano wa karibuni zaidi ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, 2024 na Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Dira ya 2050 inapaswa kuwekwa juu ya misingi kuwa CCM inaweza kuondolewa madarakani, hivyo nchi yetu inapaswa kuwa na uwezo wa kuongozwa na chama chochote kile ambacho wananchi watakichagua.

Tujenge uwiano na uwanja sawa wa kufanya siasa na kupata uongozi wa nchi, ili vyama vya siasa vibishanie mbinu tu za kutekeleza Dira ya Taifa ya 2050 kupitia ilani zao.

Mwandishi: Zitto Kabwe
Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW