Na Amiri Kilagalila
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Erasto Mpete ametoa wito kwa wananchi wa Halmashauri hiyo kujitokeza kwa wingi katika maeneo ya miradi itakayotembelewa na Mwenge wa Uhuru kesho Mei 08, 2025 ili waweze kupokea ujumbe mahususi wa Mwenge huo na kujionea utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mpete ametoa wito huo leo Mei 07, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, akieleza kuwa Halmashauri ya Mji wa Njombe inatarajia kupokea Mwenge wa Uhuru siku ya kesho ukitokea Wilayani Ludewa, ambapo utatembelea katika Kata tano.
“Mwenge wa Uhuru utapita katika Kata tano za Halmashauri ya Mji wa Njombe na utaanza kata ya Luponde kijiji cha Madobole, kwa hiyo tunaomba sana wananchi wa Madobole kujitokeza kwa wingi maana yake ndiyo sehemu ya mapokezi ili kuonyesha kwamba Halmashauri ya Mji wa Njombe tuko vizuri. Na baada ya kutoka Madobole Mwenge utakimbizwa kata ya Uwemba katika kijiji cha Ikisa na pale kutakuwa na tukio la kukagua msitu unaoitwa Ilonganjaula, na mkimbiza Mwenge atakabidhi mizinga ya nyuki” amesema Mpete.

Aidha, amesema Mwenge wa Uhuru katika Kata ya Mji Mwema utapita katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika kiwanda cha uchakataji na kusafirisha mazao ya parachichi, kituo cha afya ambapo huduma ya mionzi itazinduliwa na ugawaji wa vyandarua na bima.
Katika Kata ya Mji Mwema pia kitatembelewa kikundi cha ujasiliamali kinachojishughulisha na uchoraji, kisha Mwenge wa Uhuru utazindua madarasa sita katika Shule ya Sekondari Mpechi.
Vilevile Mpete ameongeza kuwa Mwenge wa Uhuru utatembelea Kikundi cha Wanawake na Samia, wahamasishaaji wa nishati mbadala na matumizi bora ya nishati mbadala kilichopo Njombe Mjini.
Mwenge wa Uhuru utapita katika Kata ya Ramadhani kuzindua klabu ya kupinga rushwa katika Chuo Shirikishi cha Sayansi ya Tiba, kisha utarejeshwa Njombe Mjini kwenye eneo la mkesha ambapo utafanyika uzinduzi wa gari jipya la miradi ya maendeleo.
Erasto Mpete pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha fedha kwa ajili ya miradi kwenye Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Mwandishi: Amiri Kilagalila


