Na Amiri Kilagalila
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Erasto Mpete ametoa wito kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita ambao wameanza mitihani yao leo kufanya mitihani hiyo kwa kujiamini na kupata matokeo mazuri kwa kuwa hakuna zawadi nzuri ya mtoto kwa mzazi zaidi ya kufaulu na kufanya vizuri kwenye masomo.
Mpete amezungumza hayo hapo jana mara baada ya kuwatembelea na kuzungumza na wanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Yakobi iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe ili kuwatia moyo wanapofanya mitihani yao.
“Hakuna zawadi ya maana kuliko zote kwa wazazi wenu ambayo wanafarijika wanapopewa hiyo zawadi, zawadi ambayo mnatakiwa kuwapa wazazi wenu ni ufaulu mzuri kwenye mitihani yenu ya Taifa” amesema Mpete.

Aidha, amesema kuwa Halmashauri ya Mji wa Njombe kwa sasa ina shule nne za sekondari zenye kidato cha tano na sita ikiwemo Shule ya Sekondari Yakobi, Njombe Sekondari (Njoss), Shule ya Sekondari Uwemba pamoja na Matola, na zote zimekuwa zikifanya vizuri kwenye matokeo ambapo kwa matokeo ya mwaka 2024 hazikuweza kuwa na daraja la IV wala 0.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Yakobi, Michael Uhaula ametoa pongezi kwa Mwenyekiti Erasto Mpete kwa kufika na kutoa hamasa kwa wanafunzi hao, huku akibainisha kuwa imani yake ni wanafunzi watafanya vizuri kwa kuwa shule yao imekuwa na historia ya matokeo bora.
Nao, wanafunzi wa shule hiyo wameshukuru kwa faraja ambayo wameipata kutoka kwa viongozi, ambapo wameahidi kufanya vizuri kwenye mtihani yao ambayo wameanza kufanya hii leo.
Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


