Na Dominic Allen
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu hii leo ameandika barua kulaani shambulio Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima lilitokea Aprili 30, 2025 maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam, pamoja na tukio la kushambuliwa na kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyagali lilitokea usiku wa Mei 01, 2025 akiwa katika makazi yake Iwambi, Mbeya.
“Nalaani vikali shambulio dhidi ya Padre Dkt. Charles Kitima na kushambuliwa kwa kipigo kikali na kutekwa kwa Mdude Nyagali” ameandika Lissu.
Lissu ameandika barua hiyo akiwa katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam, ambapo ametoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na serikali kuhakikisha kuwa mwanaharakati Mdude Nyagali anaachiwa huru na kupatiwa matibabu anayohitaji.
Aidha, amemtakia Padri Dkt. Kitima apone haraka, huku akiwasihi Maaskofu wa Tanzania kudumisha misimamo yao thabiti yenye misingi mikuu katika mapambano ya kudai haki, usawa na demokrasia.
“Kwa Padre Kitima, namtakia ahueni ya haraka na kumsihi yeye na Maaskofu wa Tanzania kudumisha misimamo yao thabiti na yenye misingi mikuu katika mapambano ya kudai Tanzania ya haki, usawa na demokrasia” amesema Lissu katika barua yake.

Katika barua yake hiyo, Lissu ameweka msimamo wake kuwa endapo asipopelekwa kortini siku ya Jumanne Mei 06, 2025 kama inavyostahili, ataanza rasmi mgomo wa kula.
“Nisipopelekwa kortini Jumanne kama inavyostahili, nitaanza mgomo wa kula” ameeleza Lissu.
Pia ametoa wito kwa viongozi, wanachama, wapenzi na Watanzania kwa ujumla kutokata tamaa wala kukatishwa tamaa katika kupigania demokrasia nchini Tanzania.
“Kwa viongozi wa CHADEMA, wanachama, wapenzi, na wananchi wa Tanzania kwa ujumla, nawaomba kutokata tamaa wala kukatishwa tamaa katika kupigania demokrasia ya nchi yetu” amesema Lissu.
Tundu Lissu amewahakikishia viongozi, wanachama wa CHADEMA pamoja na Watanzania kuwa yupo thabiti, hayumbishwi, na hakuna kuta za gereza zitavunja roho yake, akisema kuwa anawapenda wote na atarudi.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


