Na Amiri Kilagalila
Kufuatia changamoto ya upungufu wa nyumba ya walimu inayowakumba walimu wa Shule ya Msingi Deo Sanga iliyopo kijiji cha Manga katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho wanatarajia kukamilisha ujenzi wa nyumba pacha yenye thamani ya Tsh. Milioni 92.41.
Baadhi ya walimu hao wanaofundisha katika Shule ya Msingi Deo Sanga wamekuwa wakitembea umbali wa takribani kilomita 24 kila siku kutokana na kuishi mbali na shule hiyo.

Liston Ngimilanga ambaye ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Manga, leo Aprili 30, 2025 akitoa taarifa ya ujenzi wa nyumba hiyo mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya TASAF, Peter Ilomo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi, amesema kuwa ujenzi umefikia hatua ya umaliziaji ambapo mradi huo mpaka sasa umegharimu Shilingi 91.36.
“Katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wananchi wa kijiji cha Manga, kijiji kilipokea fedha hizo kutoka serikali kuu kupitia TASAF kwa ajili ya ujenzi wa nyumba pacha, na hii ni baada ya wananchi kuibua na kuthibitisha mradi” amesema Ngimilanga.

Nae Naboti Ilongo ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Deo Sanga, amesema mpaka sasa shule hiyo ina nyumba nne lakini mahitaji yao ni nyumba saba hivyo mara baada ya ujenzi wa nyumba hiyo kutakuwa na mahitaji ya nyumba moja.
Ilongo ameongeza kuwa baadhi ya walimu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kusafiri umbali mrefu hadi kufika shuleni hapo wakitokea mjini Makambako.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Taifa ya TASAF, Peter Ilomo amesema serikali imetoa kiasi hicho ili kuunga mkono juhudi za wananchi wa Manga ambapo amechukua nafasi hiyo kupongeza kwa usimamizi wa mradi huo.
“Jengo ni zuri na hata umaliziaji wake umefanyika kwa umahili mkubwa, na kwa kweli niwashukuru CMC kwa kusimamia hii kazi na nina imani mwezi ujao mtakuwa mmemaliza hii kazi” amesema Ilomo.

Mwandishi: Amiri Kilagalila
Mhariri: Dominic Allen


