Na Dominic Allen
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) kuendelea kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania pamoja na kuwekeza katika Hati Fungani ya Zanzibar (SUKUK).
Rais Mwinyi ametoa wito huo jana Aprili 06, 2025 akiwa mjini London nchini Uingereza alipokuwa akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini humo, ambapo amesema kuwa serikali inatambua mchango wa Diaspora katika uwekezaji nchini Tanzania pamoja na kuhamasisha utalii hapa nchini.

Aidha, amewahakikishia kuwa serikali ipo pamoja nao katika kutatua changamoto zinazowakabili kwa maendeleo ya nchi, huku akiwasisitizia juu ya kuendeleza mila na desturi nzuri za Kitanzania.

Katika mkutano huo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Uingereza (Diaspora), Rais Mwinyi pia amezindua tovuti maalum ya Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, itakayotoa fursa za kibiashara, uwekezaji, ufadhili wa elimu ya juu pamoja na ajira.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


