Na Dr. Bravious Kahyoza na Michael Kihanga
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko amezindua zoezi la mafunzo na uibuaji wa miradi yenye mvuto wa ubia (PPP) linaloendeshwa na Kituo cha Ubia (PPPC) Tanzania mafunzo yaliyofanyika katika ofisi Mkuu wa Mkoa leo.
Kituo cha Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC) kimetoa mafunzo hayo ya uibuaji wa miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP kwa Viongozi wa Mkoa na Halmashauri zake ambapo wataalam 42 wamepatiwa mafunzo hayo.
Kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mrindoko alieleza kuwa mkoa wa Katavi ni mkoa wenye fursa lukuki za kiuwekezaji ambazo zina mvuto wa ubia. Mhe. Mrindoko amezitaja fursa hizo ni kwenye sekta ya mazao ya misitu kama ufugaji wa nyuki, utalii unaoanikizwa na mbuga ya Katavi, uvuvi, usafirishaji na sekta ya kilimo.

Dr. Bravious Kahyoza (kushoto) na Michael Kihanga (kulia).
Aidha, Mhe Mrindoko amempongeza, Mhe Rais kwa jinsi alivyoimarisha uchumi. Amesema kuwa kwenye kipindi cha miaka minne, Mhe. rais Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Shilingi Trillion 1.56 kwa ajili ya shughuli za maendeleo mkoani hapo. Amesema fedha hizo zimesaidia kuimarisha sekta ya nishati ambapo zaidi ya 80% maeneo ya mjini yanapata umeme na 70% vijijini. Vilevile huduma za afya na miudombinu ya ya usafirishaji imeimarishwa.
Mhe. Mrindoka amesema kuwa hatua hizi za uwekezaji kwenye miundombinu zitakuwa muhimu kwenye miradi ya PPP mkoani Katavi.Kwa upande mwingine, Mhe. Mrindoko amempongeza Mh. rais kwa kuanzisha kituo cha ubia(PPPC) na kuitaja hatua hiyo kama hatua ya kijasiri.
Mhe. Mrindoko amesema kazi inayofanywa na kituo cha ubia chini ya Ndg. David Kafulila ni ya mfano kwani sasa dhana ya ubia inaanza kueleweka nchini.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa, Ndg. Albert Msovela amesema mafunzo hayo yatakuwa na msaada mkubwa wa mkoa wa Katavi na kusisitiza kuwa mkoa uko tayari kushirikiana na PPPC kwenye shughuli za ubia.

Mafunzo hayo,yanayoratibiwa na wakufunzi Dr. Bravious Kahyoza na Michael Kihanga yana malengo muhimu yafuatayo;
- Kuelewa dhana ya PPP na kuibua miradi yenye sifa ya utekelezwaji wa ubia.
- Kuandaa maandiko dhana (Project Concept Notes).
- Kuandaa matangazo ya miradi kwa wawekezaji.
- Kutumia teknolojia ya GIS katika uwekaji wa miradi kwenye ramani za Halmashauri.

Wakufunzi hawa baada ya kutoa mafunzo haya kwa Mkoa wa Katavi sasa wataanza kuzunguka katika halmashauri zote 6 za mkoa huo ili kuendelea kutoa mafunzo hayo.

PPPC inaendelea kutoa mafunzo katika mikoa 13 nchini kwa ajili ya uibuaji wa miradi ya PPP kwa maendeleo ikiwa ni awamu ya pili ya zoezi hili. Awamu ya kwanza ya zoezi hili lilihitimishwa mwezi Februari mwaka huu kwa wataalamu mbalimbali kupatiwa mafunzo
Mikoa ambayo zoezi hili litaendelea ni pamoja na Katavi, Mara, Rukwa, Shinyanga, Tabora, Manyara na Iringa. Mikoa mingione ni pamoja na Njombe, Ruvuma, Geita, Kagera, Lindi na Singida.
#PPPCentre #PPP #Ubia #Katavi #Uwekezaji #Mafunzo #Maendeleo
Waandishi: Dr. Bravious Kahyoza na Michael Kihanga
Mhariri: Yohani Gwangway


