Na Edward Kinabo
Msiba wa Mlandizi ni mwangwi tu wa kuwepo kwa wafu wengine wanaotembea, kwasababu ya mikopo
Mlandizi imefiwa, Tanzania imefiwa.Chanzo cha kifo ni kipigo kilichotokana na madai ya mkopo.
Watuhumiwa ni baadhi ya maafisa mikopo wa kampuni ya OYA. Lakini tatizo ni zaidi ya OYA. Tatizo ni soko holela la mikopo lisilo na uangalizi wowote makini wa kumuepusha wala kumlinda mwananchi mnyonge dhidi ya mikopo inayotolewa kiharamu na kudaiwa kikatili.
Kwasababu ya umaskini uliokithiri au dharura za kimaisha, Watanzania wengi tunalazimika kukopa, tena mikopo midogo-midogo ili kutafuta ahueni. Na kwasababu ya uelewa mdogo, mikopo imekuwa ni dili kubwa la wajanja wachache wa mjini.
Kwasababu mikopo ni siri, kumekuwa na maumivu mengi ya kisirisiri. Wengi wananyonywa kimyakimya, wanakandamizwa kimyakimya, wanatishwa kimyakimya, wanadhalilishwa kimyakimya, na wanamalizwa kimyakimya!
Ni dhahiri kuwa umaskini umezalisha biashara ya kutengeneza umaskini mkubwa zaidi kwa jina la mikopo midogo midogo (micro credits), badala ya kumkwamua mwananchi. Kwa vyovyote vile, jambo hili linahitaji mjadala wa wazi na wa kina wa kitaifa. Linahitaji ufumbuzi mpana wa kitaifa. Msiba wa Mlandizi ni mwangwi tu wa kuwepo kwa wafu wengine wanaotembea, kwasababu ya mikopo.
Wajanja wanafanyaje?
Pata mtaji kidogo, sajili kampuni, vuta leseni na vibali vya kazi, kisha nenda zako kwa wananchi! Utaruhusiwa kirahisi sana kukopesha wananchi. Kisa? Umesajiliwa, una leseni na unalipa kodi!
Sasa ukiondoa sheria, kanuni, viwango na masharti yaliyowekwa huko juu, huku chini walipo wananchi ni kweupe kabisa. Hakuna uangalizi wa kutosha, hakuna ukaguzi, hakuna uhakiki wa kutosha wa mikopo mahsusi wanayotoa, viwango vya riba wanavyotumia, dhamana wanayowekeza wala mfumo wa marejesho wanaoutumia. Uchochoro ni mwingi sana.
:Chanzo cha tatizo
- Tuna sheria, kanuni na miongozo inayosimamia huduma za mikopo ya Microfinances, chini ya usimamizi wa BoT na mamlaka mbalimbali; taratibu ambazo zingesimamiwa vizuri, angalau zingeweza kumnusuru na kumlinda mwananchi.
- Tatizo ni kwamba, viongozi wengi (siyo wote) katika mikoa, wilaya na halmashauri (huku walipo wananchi), hawazijui kabisa “instruments hizo”, na wala hawajishughulishi kuzijua.
- Kigezo pekee kinachotumika kuzikaribisha au kuziruhusu kampuni za mikopo kuanza kukopesha wananchi huku chini ni vyeti na vibali vyao vya usajili tu…basi.
- Suala la mikopo limechwa liwe ni suala la mkopaji na mkopeshaji. Kwamba, watajuana wenyewe. Hapo ndipo baadhi ya “Microfinances” zinapopata uchochoro wa kufanya ulaghai, kumnyonya na kumkandamiza mwananchi. Na hapo ndipo wananchi wengi wasio na uelewa wa kutosha huingizwa mjini.
- Microfinances nyingi (siyo zote) hutumia vibaya umaskini wa wananchi, unyonge na uelewa wao mdogo kuwashawishi kukopa, kuwaongezea gharama za mkopo kupitia ada za forms, kuwawekea riba kubwa kupindukia, muda mfupi wa marejesho, kuweka rehani dhamana ambazo hazina uwiano na mkopo husika, na wakati mwingine hukamata hata mali nyingine za wananchi zisizohusika. Kuna udhalilishaji mpys umeingia. Ni namba zote za simu ulizonazo kutumiwa messages zinazofichua kuwa unadaiwa!
- Usajili, leseni na vibali vingine vya kikazi, bado havijatosha kuzuia Microfinances kupindisha Sheria, Kanuni na Taratibu hasa kufanya janjajanja kwenye eneo la riba, marejesho na dhamana, ili kujitengenezea faida haramu na za haraka. Kwa bahati mbaya, katika maeneo hayo nyeti, hakuna Kiongozi wala Jicho lolote la kumuepusha au kumlinda huyu mwananchi mnyonge, mwenye uelewa mdogo.
- Matokeo yake ni kukithiri kwa mikopo mingi laghaifu, lazimishi na isiyolipika, na wakopaji kushughulikiwa isivyo halali huku wakiwa hawajui pa kukimbilia.
Nini kifanyike
Mikopo ni huduma nzuri inapozingatia sheria, kanuni na taratibu, na inapoitikia vizuri hali za walaji (wateja). Zipo Microfinances chache zilizowaokoa na kuwanyanyua wananchi kupitia mikopo.
Hata hivyo, soko holela la mikopo linahitaji uangalizi na udhibiti wa kina zaidi ili kumlinda mwananchi dhidi ya Microfinances zinazofanya vibaya.
Kunahitajika Jicho la Mikopo (Loans Watch). Huduma ya kutoa elimu rahisi kuhusu mikopo, kufanya uchunguzi, ukaguzi, uhakiki, mapitio, mashauriano, ushauri na utetezi wenye nia ya kumuepusha au kumlinda mwananchi dhidi ya mikopo ya kihuni na kikatili.
Kama angalau, miongozo na masharti ya BoT kuhusu mikopo hii, ingewekwa wazi zaidi na kutolewa elimu rahisi kwa wananchi, basi wengi wangenusurika.
Binafsi, nimewahi kuwanusuru wananchi wawili waliokuwa kwenye mikopo kandamizi sana ya Microfinances. Kwa kutumia miongozo ya BoT niliweza kuzungumza na Wakurugenzi wa Microfinances husika na kuwaonesha jinsi walivyokuwa wanafanya unyonyaji na ukandamizaji katika riba na mfumo wao wa madai. Na kwasababu ya aibu na hofu ya kuchukuliwa hatua za kisheria, Wakurugenzi wale, kila mmoja kwa kesi yake na kwa wakati wake, waliomba radhi na kufuta uonevu wote waliokuwa wameufanya. Tukamalizana nao kimyakimya.
Lakini ni dhahiri kuna wananchi wengi zaidi wamenyonywa na kukandamizwa sana kupitia kampuni hizo mbili. Achilia mbali baadhi ya Microfinances nyingine.
Ni kama vile suala la unyonyaji na ukandamizaji kaachiwa mwananchi mwenyewe. Kwamba likitokea, sheria zipo basi mwananchi achukue hatua. Lakini ukweli ni kwamba wananchi wetu wengi hawana uelewa, uwezo wala uthubutu wa kuchukua hatua. Wanakufa nayo kimyakimya.
Ni maoni yangu kuwa kunahitajika Jicho la Mikopo (Loans Watch), yaani huduma itakayotoa elimu, tahadhari, ukaguzi, uhakiki, mapitio, mashauriano na uangalizi wa kina na wa mara kwa mara kwenye sekta nzima ya mikopo, hususan kwenye mikopo mahsusi inayotolewa ili kumuepusha au kumnusuru mwananchi dhidi ya unyonyaji, ukandamizaji na udhalilishaji.
Aidha, kunahitajika mjadala mpana zaidi wa kitaifa kuhusu madhila ya mikopo ili kupata ushauri na ufumbuzi zaidi wa suala hili.
Kinyume na hapo, huduma nyingi za mikopo zitaendelea kutengeneza umaskini zaidi, kusababisha misongo ya mawazo na hata maafa kwa wananchi. Inawezekana kuepusha yote hayo. Tuchukue hatua.
Mwandishi: Edward Kinabo
Mhariri: Yohani Gwangway
Kuhusu Mwandishi
Edward Kinabo ni Mfanyabiashara, Mchambuzi wa Masuala ya kijamii na kisiasa na Mwanaharakati wa Haki na Maendeleo ya Binadamu. Anapatikana kwa simu: 0623003438.


