Land Dwellers inalaani kitendo cha Jeshi la Polisi Tanzania kuwafukuza waandishi wa habari waliokuwa wanatekeleza majukumu yao katika Makao Makuu ya CHADEMA, Mikocheni jijini Dar es Salaam hii leo.
Waandishi hao wa habari walifika katika ofisi hizo kufuatia wito wa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika aliyetaka kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari, lakini katika hali ya kustaajabisha askari wa Jeshi la Polisi waliwafukuza waandishi hao.
Land Dwellers inalaani vikali kitendo hicho kilichofanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya waandishi hao wa habari waliokuwa wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Ibara ya 18 (1) inavyoelekeza, na pia kulitaka Jeshi hilo kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Vilevile Land Dwellers inatoa wito kwa taasisi za zinahusika na waandishi wa habari pamoja na zile zinazotetea haki za binadamu kutofumbia macho kitendo hicho cha Jeshi la Polisi kwani kinakiuka misingi ya haki za binadamu.


