Misitu yetu, mustakabali wetu: Vita dhidi ya upotevu wa misitu Tanzania

Na Dominic Allen

Leo, Juni 05, 2026 Watanzania wameungana na ulimwengu mzima kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani chini ya kauli mbiu isemayo, “Imechochewa na Asili. Kwa Tabianchi. Kwa Mustakabali Wetu.” Kauli hii ikitukumbusha kuwa suluhisho la changamoto nyingi za mazingira na mabadiliko ya tabianchi linapatikana katika kulinda na kurejesha mifumo ya asili inayotegemewa na viumbe hai pamoja binadamu, ambapo misitu ni moja ya kiungo muhimu.

Misitu imekuwa uti wa mgongo wa ustawi wa mazingira, uchumi na maisha ya watu kwa miongo mingi, ikiwa ni nguzo katika kuhifadhi bioanuwai, kulinda vyanzo vya maji na kusaidia jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, bado tatizo la upotevu wa misitu limeendelea kuikabili dunia nzima, kwa mujibu wa chapisho la Umoja wa Mataifa (UN) la Mei 12, 2026, dunia ilipoteza wastani wa hekta milioni 10.9 za misitu kila mwaka kati ya 2015 na 2025.

Hata hivyo, kutokana na juhudi za upandaji miti na urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa, upotevu halisi wa misitu ulipungua hadi wastani wa hekta milioni 4.12 kwa mwaka.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya nchi, dunia bado inaendelea kupoteza sehemu kubwa ya misitu yake kila mwaka.Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye rasilimali kubwa za misitu barani Afrika, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya upotevu wa misitu. Mnamo Septemba 2024, akitoa taarifa Bungeni jijini Dodoma, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula alisema Tanzania ina jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu, ikijumuisha misitu inayosimamiwa na serikali pamoja na watu au sekta binafsi.

Kitandula alieleza kuwa Tanzania inapoteza wastani wa hekta 469,000 za misitu kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kilimo kisicho endelevu, moto, shughuli za ufugaji na ukataji wa miti. Kiwango hicho kinaashiria kuwa pamoja na jitihada zinazoendelea za uhifadhi na upandaji miti, bado kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa misitu na kuhamasisha matumizi endelevu ya ardhi ili kuzuia kuendelea kupungua kwa uoto wa asili nchini.

Ukubwa wa tatizo la upotevu wa misitu sio tishio kwa mazingira pekee, bali pia kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani kadri misitu inavyopungua, ndivyo uwezo wake wa kufyonza hewa ya ukaa unavyopungua, hali inayochangia kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Athari za ukataji misitu zinaonekana wazi katika maeneo mengi nchini. Mabadiliko ya mifumo ya mvua, ukame wa mara kwa mara, kupungua kwa vyanzo vya maji na kuongezeka kwa joto ni baadhi ya matokeo yanayohusishwa na kupungua kwa uoto wa asili. Kwa jamii zinazotegemea kilimo na ufugaji, athari hizi zina maana ya kupungua kwa uzalishaji na kuongezeka kwa umaskini.

Takwimu zilichochapishwa kwenye tovuti ya Shirika la Global Forest Watch zinaonesha kuwa Tanzania ilipoteza hekta milioni 3.7 za uoto wa miti kati ya mwaka 2001 na 2025. Upotevu huo pia ulihusishwa na utoaji wa takribani gigatani 1.3 za hewa ukaa (CO₂e), hali inayoonesha jinsi ukataji na uharibifu wa misitu unavyochangia kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi nchini na duniani.

Kutokana na hali hiyo, serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na misitu. Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani mwaka 2025 yaliyofanyika mkoani Njombe, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisisitiza dhamira ya Tanzania katika kuhifadhi misitu, ambapo pia alizindua kampeni ya upandaji wa miti, ili kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na ukataji wa misitu.

Katika kukabiliana na changamoto ya ukataji misitu, serikali imeendelea kuwekeza katika kampeni za upandaji miti kama sehemu ya mkakati wa kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na kuongeza uoto wa asili nchini. Kupitia kampeni ya Tanzania ya Kijani, Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka msisitizo mkubwa katika uzalishaji na upandaji wa miche ya miti ili kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za misitu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza bungeni Mei 2026 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema serikali ilikuwa imepanga kuzalisha na kupanda miche ya miti milioni 35.2 katika mwaka wa fedha 2025/26.

“Hadi kufikia Aprili 2026, Wizara imezalisha miche ya miti milioni 32.8 ya aina mbalimbali ambayo imeendelea kupandwa katika mashamba 26 ya Serikali na kugawanywa kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao,” alisema Dkt. Kijaji.

Akiongeza kuwa hatua hiyo imechochea na kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la upandaji miti na uhifadhi nchini Tanzania.

Takwimu hizi zinaonesha kuwa pamoja na changamoto ya upotevu wa misitu, bado serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi za kuongeza eneo la misitu nchini kupitia ushirikishwaji wa wananchi, taasisi za umma na sekta binafsi. Mafanikio ya kampeni hizi yatakuwa muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kulinda vyanzo vya maji na kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kuelekea uchumi wa kijani.

Pamoja na changamoto za upotevu wa misitu zinazolikabili taifa, sekta ya misitu imeendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi kupitia uzalishaji wa malighafi, viwanda vya kuongeza thamani na biashara ya mazao ya misitu ndani na nje ya nchi. Takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii za mwaka 2025 zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uzalishaji wa malighafi za mbao katika mashamba ya Serikali yanayolimwa miti kibiashara umeongezeka kutoka mita za ujazo 1,108,791 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi mita za ujazo 1,264,535 mwaka 2024/2025.

Aidha, idadi ya viwanda vya kati na vikubwa vya kuongeza thamani mazao ya misitu imeongezeka kutoka 636 mwaka 2020 hadi 1,671 mwaka 2025, huku viwanda vidogo vidogo kama useremala vikizidi 7,000 nchini. Sambamba na mafanikio hayo, thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 105.7 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 458.5 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 333.8. Takwimu hizi zinaonesha kuwa misitu si rasilimali muhimu kwa mazingira pekee, bali pia ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi, ajira na maendeleo endelevu ya Tanzania.

Mbali na kampeni za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, Tanzania pia imeweka misingi wa kisheria inayolenga kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, ambayo inasisitiza kuwa uhifadhi wa mazingira si jukumu la Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi. Sheria hiyo inatambua kuwa mafanikio ya juhudi za kukabiliana na changamoto za mazingira, ikiwemo ukataji misitu, yanategemea ushiriki wa wananchi katika kutunza na kulinda mazingira yanayowazunguka.

“Mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira,” kimeeleza kifungu cha 6 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

asharti hayo yanaweka wazi kuwa mapambano dhidi ya ukataji holela wa miti na uharibifu wa mazingira kwa ujumla ni jukumu la pamoja. Hivyo, pamoja na uwepo wa taasisi za serikali zinazosimamia misitu na mazingira, wananchi nao wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali hizo kwa kuripoti vitendo vya uharibifu wa mazingira, kushiriki katika upandaji miti na kutumia rasilimali za asili kwa njia endelevu.

Juhudi za kukabiliana na ukataji misitu nchini pia zinaongozwa na Mpango wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu wa mwaka 2021–2031, ambao unaweka dira ya muda mrefu ya usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za misitu nchini. Kupitia mpango huo, serikali imelenga kuhakikisha sekta ya misitu inachangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo endelevu ya taifa huku ikihakikisha rasilimali za asili zinahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Kuongeza mchango wa sekta ya misitu katika maendeleo endelevu ya Tanzania na uhifadhi pamoja na usimamizi wa rasilimali zake za asili kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” umebainisha mpango huo.

Dhamira hiyo inaonesha kuwa misitu haitazamwi tu kama chanzo cha malighafi au mapato ya kiuchumi, bali pia kama urithi muhimu unaopaswa kulindwa ili kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuwai na kulinda vyanzo vya maji kwa maendeleo ya muda mrefu ya nchi.

Pamoja na uwepo wa sheria na sera hizo, changamoto bado ipo. Mahitaji makubwa ya mkaa na kuni kama chanzo cha nishati kwa mamilioni ya Watanzania yanaendelea kuwa sababu kubwa ya ukataji wa miti. Ukuaji wa idadi ya watu, ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo na makazi pamoja na ukataji haramu wa miti navyo vinaongeza shinikizo kwa misitu iliyopo.

Kadri dunia inavyoendelea kukabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, umuhimu wa misitu unaongezeka zaidi. Misitu si mapambo ya mazingira, bali ni ngao dhidi ya ukame, mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na ongezeko la joto duniani. Kuendelea kuikata bila kuirejesha ni sawa na kuharibu msingi wa maendeleo ya baadaye.

Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, maadhimisho haya kitaifa yanafanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, yakiwa Kauli Mbiu “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.” Mgeni rasmi ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Hata hivyo, mafanikio ya vita dhidi ya ukataji misitu hayatapatikana kwa juhudi za serikali pekee, kuna haja ya kuimarisha utekelezaji wa sheria za mazingira na misitu, kuongeza uwekezaji katika uhifadhi wa misitu na kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni. Kadhalika, mipango ya upandaji miti inapaswa kupewa kipaumbele zaidi ili kuhakikisha maeneo yaliyoharibiwa yanarejeshwa, na rasilimali za misitu zinaendelea kunufaisha taifa kwa muda mrefu.

Kwa upande wa sekta binafsi, huu ni wakati wa kutambua kuwa ukuaji wa uchumi na uhifadhi wa mazingira ni mambo yanayopaswa kwenda sambamba, kampuni na taasisi zinapaswa kuongeza uwekezaji katika miradi ya urejeshaji wa misitu, kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na kuhakikisha shughuli zao za uzalishaji haziendelei kuchangia uharibifu wa misitu. Ushiriki wa sekta binafsi unaweza kuwa nguvu kubwa katika kufanikisha ajenda ya Tanzania ya Kijani na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wananchi pia wanao wajibu wa kulinda misitu unaanzia katika maamuzi ya kila siku tunayofanya. Kupanda na kutunza miti, kulinda vyanzo vya maji, kutumia rasilimali za asili kwa uangalifu na kutoa taarifa juu ya vitendo vya uharibifu wa mazingira ni miongoni mwa hatua zinazoweza kuleta mabadiliko makubwa kwa taifa. Tukichukua hatua leo, tutakuwa si tu tunalinda mazingira yetu, bali pia tunajenga msingi imara wa maendeleo, ustawi na usalama wa vizazi vijavyo.

Mwandishi: Dominic Allen

Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW