Na Fredrick M. Justine
“Kwa uhuru mlitwaliwa. Basi simameni imara, wala msiweke tena shingoni nira ya utumwa.” — Wagalatia 5:1
Katika historia ya mataifa mengi, nyakati za dhuluma, unyanyasaji na mateso huwa ndio ngazi ya kuinuka kwa ujasiri wa pamoja. Lakini kuna nyakati kama ilivyo sasa kwa Tanzania, ambapo watu huonekana kana kwamba wanakubali kunyanyaswa, wanakubali kufungwa na wanakubali kimya kimya kuporwa utu na haki zao. Swali linalojitokeza: Kwanini tunashindwa kusimama na kuchagua njia ya haki, hata tunapoumia?
“Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi hali ya watu mpaka wabadilike yaliyo ndani ya nafsi zao.” — Qur’an 13:11
Misri ya kijamii, kisaikolojia na kisiasa
Watanzania wengi wanaishi katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni “Misri” ya sasa: Mazingira ya unyonge, umaskini, unyanyasaji wa wazi wa haki za binadamu, utekaji, kukamatwa holela kwa wanaharakati na hata vifo vya raia vinavyofunikwa kwa propaganda.
Katika Biblia (Kutoka 3–14), Wana wa Israeli walikuwa watumwa chini ya Farao, na ingawa walikuwa wakilia kwa mateso yao, bado walihitaji nguvu ya ziada ya kiakili na kiroho kukubali kuondoka. Walihitaji mwanzo mpya na kumwamini Mungu kuliko Farao.
Hali hiyo inaakisi Tanzania ya leo. Ingawa tunajua mateso tunayopitia, bado tunasita kuvunja minyororo ya hofu, ukondoo wa kisiasa na ukimya wa kitaifa.
Hofu imekuwa ibada mpya
Katika Qur’an, tukio la Musa na Firauni linatajwa mara nyingi, lakini moja ya sehemu zenye kuamsha tafakuri ni pale Firauni alipowatisha watu wake kwa nguvu za dola na udhibiti wa maisha yao.
“Firauni akasema: Mimi nawaogopesha kwa moto! Lakini Musa akamwambia: Haki imekuja kutoka kwa Mola wenu. Na Firauni hakutaka kusadiki.” — (Qur’an 40:49-50, muhtasari)
Firauni wa sasa hajavaa taji la dhahabu wala kushika fimbo ya kifalme. Anaweza kuwa kiongozi wa taasisi, mtawala wa serikali au hata mfanyabiashara mkubwa anayenunua haki kwa pesa. Hofu inayotandazwa na mifumo hii imewafanya watu kuabudu kimya na kutukuza udhalimu kwa jina la “amani.”
Je, tumekuwa wafungwa wa hekaya za uwoga?
Katika fasihi ya Kiafrika, Ngugi wa Thiong’o aliwahi kusema, “Silaha kuu ya mdhalimu ni akili ya aliyedhulumiwa.”
Maneno haya yana uzito mkubwa leo, kwani tunaona mifumo ya kisiasa ya ukandamizaji inawafanya wananchi waamini kuwa hakuna njia nyingine isipokuwa kunyenyekea. Wamefundishwa kuwa mabadiliko ni machafuko, na utii ni hekima. Huu ni uongo mkubwa wa kihistoria.
Kama alivyoandika Shaaban Robert katika Wasifu wa Siti binti Saad, “Binadamu hufanywa si kwa sura bali kwa msimamo.” Je, tuna msimamo gani kama taifa mbele ya unyanyasaji wa wenzetu?
Sisi ni Musa wa wakati huu
Hatutegemei tena Musa atoke jangwani, sisi ndio Musa wa wakati huu. Sauti za wananchi, wanaharakati, walimu, waandishi wa habari, viongozi wa dini pamoja na vijana ndizo zenye uwezo wa kusema “Achilia watu wa Mungu waende.”
Lakini haya hayawezi kutokea bila mabadiliko ya ndani kama maandiko yote mawili yanavyofundisha:
“Badilikeni kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu.” — (Warumi 12:2)
“Mwenyezi Mungu hawabadilishii watu hali yao mpaka wabadilike wao wenyewe.” — (Qur’an 13:11)
Huu ni wito kwa mtu binafsi, iwe ni kiongozi wa Chama Tawala au Upinzani, badilika wewe kabla hujalalamika kwa nini Taifa halibadiliki.
Haki haitolewi, hulazimishwa kwa ustaarabu, nguvu au kususia
Tanzania haihitaji mapinduzi ya silaha, bali ya fikra. Inahitaji watu wanaothubutu kuuliza maswali magumu, wanaokataa kula matapishi ya ahadi hewa kila baada ya miaka mitano, na wanaojua kuwa haki haiji kwa kusubiri bali huletwa kwa hatua, kwa mshikamano na kwa kujitoa.
Ni wakati wa kutoka Misri, si tu ya kiuchumi, bali ya kiakili na kiroho. Haki haijawahi kuwa zawadi; ni tunda la kusimama imara.
“Na mtajua kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” — Yohana 8:32
“Wala msiwe dhaifu wala msihuzunike, na ninyi mtakuwa juu ikiwa nyinyi ni waumini wa kweli.” — Qur’an 3:139
Mwenye sikio na Asikie.
Mwandishi: Fredrick M. Justine
Mhariri: Dominic Allen


