Na Dominic Allen
China imesema kuwa haitokubali kushurutishwa na Marekani kufuatia vita vya kibiashara vilivyochochewa na ushuru uliyowekwa na Rais Donald Trump kwa bidhaa zinazoingia nchini Marekani, jambo lililopelekea kuyumba kwa masoko ya hisa.
Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Wang Wentao ametoa msimamo huo leo baada ya Rais Trump kutishia kuongeza ushuru kwa zaidi ya asilimia 100 kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka kwenye taifa hilo ambalo ni la pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani, ikiwa ni kujibu uamuzi wa Beijing wa kuweka ushuru wa ‘kisasi’ dhidi ya bidhaa za Marekani, kufuatia hatua ya awali ya Trump aliyotangaza juma lililopita.
“Kitisho cha Marekani kuongeza ushuru dhidi ya China ni kosa juu ya kosa, na kwa mara nyingine kinadhihirisha tabia ya ushurutishaji ya Marekani,” amesema Wentao
“Marekani ikisisitiza kutekeleza matakwa yake, China itapigana hadi mwisho,” ameongeza Wentao
Mwandishi: Dominic Allen


