Na Dominic Allen
Wanachama wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (NETO) wamesema kuwa hawawatambui wanaojiita viongozi wa umoja huo ambao Machi 12, 2025 walienda jijini Dodoma kukutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Wanachama hao kupitia taarifa waliotoa hii leo kwa umma, wamelaani na kujitenga na misimamo ambayo wamekuja nayo viongozi hao, wakisema kuwa wamefanya kinyume na maazimio na mienendo ya NETO.
Katika taarifa hiyo wanachama hao wamebainisha kuwa wameamua kuanzisha vuguvugu jipya la harakati za kudai ajira kwa walimu nchini ambalo linaitwa ‘NETO Members Movement (NETO-MEMO).
Ikumbukwe kuwa mnamo Machi 12, 2025 baada ya viongozi hao wa NETO wakiongozwa na Mwenyekiti wa umoja huo, Joseph Kaheza kukutana na Mawaziri hao, Waziri George Simbachawene aliagiza kuundwe timu ya wataalamu itakayochambua waraka wa NETO, ili mapendekezo yao yatumike kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa walimu.
Hatua hiyo imepingwa vikali na wanachama wa umoja huo ambao kwa sasa wamejitenga na kuanzisha umoja mwingine, wakisema kuwa hapo awali msimamo wao ulikuwa ni kuitaka serikali ikutane na walimu wote wasio na ajira nchini ambao ndiyo wahanga, hivyo waliokwenda Dodoma walilazimisha kwenda.
Hata hivyo Umoja huo mpya wa NETO Members Movement (NETO-MEMO), umeitaka serikali kutoa ajira kwa walimu kabla ya kuvunjwa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


