Utafiti mpya: Miradi ya Kaboni tishio kwa jamii za asili Tanzania

Na Dominic Allen

Muungano na Mshikamano wa Kimataifa wa Wamasai (MISA) hapo jana Machi 11, 2025 ulizindua ripoti maalum ambayo imefanya uchunguzi wa kina kuhusu miradi ya kaboni Kaskazini mwa Tanzania. Kwa mujibu wa ripoti ya MISA, miradi hiyo inaweza kupelekea wananchi wa maeneo hayo kunyang’anywa maeneo yao, vile vile kuleta athari kubwa kwa jamii za kifugaji.

MISA imechambua kwa kina Mradi wa Kaboni wa Maeneo ya Malisho wa Longido na Monduli (LMRCP) unatekelezwa na Soil For Future Ltd, na Mradi wa Ikolojia Imara Tarangire (RTEP) ambao upo chini ya The Nature Conservancy (TNC), ukilenga wilaya tatu ambazo ni Longido, Monduli na Simanjiro.

Ripoti ya MISA, imebaini kuwa hakukuwa na uwazi kuhusu mikataba iliyosainiwa ya miradi hiyo, ushirikishaji hafifu kwa jamii kuhusu kuanzishwa kwa miradi hiyo, pamoja na kutengwa kwa vijana na wanawake. Hii imepelekea jamii kukosa uelewa wa msingi kuhusu masoko ya kaboni, masharti ya mkataba na athari zake kwa mazingira na jamii kwa ujumla.

“Wanajamii mara nyingi hawana uelewa wa msingi kuhusu nasoko ya kaboni, masharti ya mikataba na athari zake” imesema ripoti hiyo.

Miradi hiyo ya kaboni inahofiwa kuharibu mfumo wa ufugaji kwa jamii za kiufugaji, ambapo jamii za kifugaji zina desturi ya kuhama mara kwa mara kutokana na asili ya maisha yao, lakini miradi hii inaleta mifumo ya malisho ya mzunguko ambayo inazuia mifumo ya jadi ya malisho jamii ya kimasai.

“Mabadiliko haya yanahatarisha usalama wa chakula na mikakati ya jamii kuhimili mabadiliko ya tabianchi” imeeleza ripoti hiyo.

Uchunguzi wa MISA umeeleza kuwa kanuni za biashara ya kaboni nchini Tanzania hazina masharti madhubuti kulinda haki za binadamu hasa kwa jamii za asili, jambo linalosababisha upotoshaji ndani ya jamii, rushwa pamoja na utata wa kisheria hasa kuhusu usitishaji wa mikataba na mifumo ya mgawanyo wa faida.

“Ukosefu wa mfumo wa kisheria uliyowazi ba wa lazima umesababisha upotoshaji wa jamii, ufisadi na utata wa kisheria” Ripoti ya MISA imebainisha hayo.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa jamii za kimasai zimejikuta katika shinikizo la kuingia kwenye mikataba kutokana ushindani uliyopo baina ya waendeshaji wa miradi hiyo miwili ili kufikia viwango vya kimataifa, ambapo waendeshaji wa miradi hiyo wanatakiwa kusaini mikataba na idadi ya fulani ya vijiji, kukamilisha nyaraka za miradi yao na kuonesha ushahidi wa idhini kutoka kwa wananchi.

“Jamii zina hofu juu ya vikwazo vya muda mrefu vya matumizi ya ardhi, kupoteza maeneo ya malisho pamoja na migogoro ndani na baina ya jamii, pamoja na mmomonyoko wa tamaduni zao” imesema ripoti hiyo.

MISA imetahadharisha kuwa huenda historia ya kunyang’anywa ardhi kwa jamii ya kimasai ikajirudia, ambapo ardhi huishia kwenye umiliki wa wawekezaji wa kigeni pamoja na maeneo yao ya malisho kubinafsishwa.

Baada ya MISA kufanya uchunguzi  huu wa kina kuhusu Mradi wa Kaboni wa Maeneo ya Malisho wa Longido na Monduli (LMRCP) unaotekelezwa na Soil For Future Ltd, na Mradi wa Ikolojia Imara Tarangire (RTEP) ambao upo chini ya The Nature Conservancy (TNC), imetoa mapendekezo kadhaa.

MISA imependekeza kusitishwa kwa muda wa miaka mitano kwa miradi yote ya kaboni kwenye udongo katika maeneo ya malisho ya kimasai, ili kutoa nafasi ya elimu kwa jamii pamoja na kuandaliwa kwa mifumo thabiti ya kisheria  katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

“Zuio la miaka mitano ni muhimu ili kulinda haki za wamasai na mifumo yao ya ufugaji katika matumizi ya ardhi” imeshauri ripoti hiyo.

Vilevile Ripoti imesisitiza juu kutengeneza mfumo maalum wa kisheria kwa miradi ya kaboni kwenye udongo, kuhakikisha ulinzi wa haki za binadamu na haki za ardhi kwa jamii za asili.

“Kuandaliwa kwa mfumo maalum wa kisheria wa Tanzania kwa miradi ya kaboni kwenye udongo, kuhakikisha ulinzi wa haki za ardhi za jamii za asili na haki za binadamu” imeeleza ripoti ya MISA

Ushiriki wa jamii katika mchakato wa maamuzi yote umetiliwa mkazo katika ripoti ya MISA, ambapo imesema kuwa vijana, wanawake, makundi maalum pamoja wananchi wote wa vijiji husika kushirikishwa kikamilifu. Pia imetaka kuwepo kwa ushauri huru usio na upendeleo kuhusu miradi ya kaboni na athari zake.

MISA imetaka uendeshwaji wa miradi ya kaboni iheshimu mifumo ya malisho ya jadi ya Wamasai, pia miradi haitakiwi kuzuia mfumo wa asili wa wamasai wa kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine. Vilevile ripoti imesisitiza juu ya ushirikiano wa maeneo ya malisho hasa nyakati za ukame.

“Miradi ya kaboni lazima iheshimu mifumo ya malisho ya jadi ya kimasai na kudumisha udhibiti wa jamii juu ya matumizi ya ardhi…miradi haitakiwi kuzuia uhamaji wa wafugaji” imesema ripoti hiyo.

Ripoti ya MISA pia imetaka mikataba ya miradi ya kaboni iwe ya wazi na haki, iandikwe kwa lugha ya wenyeji na pia isiwe na upendeleo kwa maslahi ya waendeshaji wa miradi hiyo na serikali.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW