Na Dominic Allen
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano yanayoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kati ya wapiganaji wa Kundi la M23 na Jeshi la DRC katika mji wa Goma.
Wito huo umetolewa baada ya kufanyika kikao cha dharura kilichoitishwa hapo jana Januari 29, 2025 na Mwenyekiti wa EAC ambaye ni Rais wa Kenya, William Ruto.
Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki chini ya Rais Ruto wametoa wito huo wa kusitishwa mapigano hayo pamoja na kulinda balozi za kidiplomasia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Katika hatua nyingine, walihimiza pande zinazokinzana kuruhusu upatikanaji wa msaada wa kibinadamu kwa raia wanaoathiriwa na vita hivyo.
“Mkutano huo pia ulieleza wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mgogoro unaojitokeza kupitia mashambulizi dhidi ya ofisi za ubalozi na wafanyakazi walioko Kinshasa. Kwa hiyo, mkutano ulihimiza serikali ya DRC kulinda balozi za kidiplomasia, maisha na mali.” Sehemu ya tamko kutoka kwenye mkutano huo.
Viongozi hao pia walimhimiza Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi kujadiliana na kundi la M23 na makundi yote yenye silaha pamoja na wadau wengine muhimu ili kufikia suluhisho la amani kwa mzozo huo.
Licha ya kikao hicho cha dharura kuhusu machafuko yanayoendelea huko Goma, lakini Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), Felix Tshisekedi na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye hawakushiriki katika kikao hicho.
Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa tangu mwanzoni mwa juma hili, mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi pamoja na washirika wake huko Goma yamesababisha vifo vingi vya raia na hospitali kujaa majeruhi.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


