Na Dominic Allen
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, amesema kuwa noti mpya za Tanzania zenye saini za Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba na yeye mwenyewe zitaanza kutumika kuanzia Februari 01, 2025 sambamba na noti zingine za toleo la mwaka 2010 ambazo tayari zipo kwenye mzunguko.
Gavana amesema hayo wakati akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Zanzibar (Fedha na Mipango), Dkt. Saada Mkuya, noti za kifani za shilingi 10,000, 5,000, 2,000 na 1,000.
“Mheshimiwa Waziri, tunatarajia noti hizi zitaingia kwenye mzunguko tarehe 1 Februari mwaka huu na katika kuzisambaza tunawafahamisha wananchi kwamba noti hizi zitaendelea kutumika sambamba na noti zilizopo kwenye mzunguko” amesema Gavana Tutuba.

Gavana Tutuba alifafanua kuwa noti hizo zina mwonekano sawa na noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa mwaka 2010, zikiwa na alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine isipokuwa tu kwenye saini ya Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Waziri wa Fedha wa sasa, Dkt. Mwigulu Nchemba na saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania mstaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Gavana wa sasa wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba” aliongeza Gavana Tutuba.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dkt. Mkuya, amemshukuru Gavana na kumpongeza kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa na kwa kuendelea kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya fedha.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


