Takriban watu 12 wameuawa na wanamgambo wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo usiku wa Disemba 31, 2024 na Januari 01, 2025.
Vyanzo vya kuaminika vililiambia Shirika la habari la AFP kuwa waasi wa ADF waliwaua watu wanane katika kijiji cha Bilendu na kuua wengine wanne katika kijiji cha Mangoya na kisha kuchoma nyumba zao.
Huu ni mfululizo wa mauaji ya raia nchini humo, ambapo siku ya Sikukuu ya Krismasi mwaka jana waasi hao waliua takriban watu 21 kaskazini mwa eneo la Kivu.
Kundi la waasi la ADF ambalo asili yake ni Uganda, liliingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo miaka ya 1990 na kukita mizizi maeneo ya kaskazini ambapo hadi leo limeshaua maelfu ya raia nchini humo.


