Na Dominic Allen.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa leo Disemba 19, 2024 amesema kuwa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) umeendelea kuimarika kwani katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 hadi Novemba 2024 kiwango cha shehena kilichohudumiwa na Bandari zote zilizopo chini ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni tani milioni 16.5 ambacho kimeongezeka kwa asilimia 5.2, kulinganisha na kiwango cha tani milioni 15.6 cha shehena kilichohudumiwa kati ya mwezi Mei 2023 hadi Novemba 2023.
Msigwa amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia kuhusu utendaji kazi wa TPA. Msigwa amesema bandari zote nchini zilizopo chini ya TPA pia zilifanikiwa kuhudumia idadi ya makasha 621,584 ambapo kuna ongezeko za asilimia 3.29 ikilinganishwa na idadi ya makasha 601,805 yaliyohudumiwa kati ya mwezi Mei 2023 hadi Novemba 2023.
Bandari ya Dar es Salaam pekee, kati mwezi Mei, 2024 hadi Novemba 2024 kiwango cha shehena tani milioni 14.4 ilihudumiwa na bandari hiyo ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.6, ikilinganishwa na shehena tani milioni 13.7 iliyohudumiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Kwa upande mwingine, Bandari ya Dar es Salaam imefanikiwa kuhudumia idadi ya makasha 598,672 ikilinganishwa 597,613 yaliyohudumiwa mwaka jana katika kipindi kama hicho.
Bandari ya Dar es Salaam pia katika kipindi hicho cha mwezi Mei hadi Novemba mwaka kuu, takriban tani milioni 6.3 za shehena kutoka nchi jirani zimehudumiwa na bandari hiyo, ambayo ni sawa na asilimia 19.3 ya ongezeko la shehena zilizokwenda nchi jirani ikilinganishwa na mwaka 2023 kipindi kama hicho ambapo ilikuwa ni tani milioni 5.3 za shehena kutoka nchi jirani.
Katika hatua nyingine Gerson Msigwa amesema kwa sasa meli za shehena katika Bandari ya Dar es Salaam kwa wastani husubiri kwa siku 7 kushusha mizigo ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo zilikuwa zinasubiri hadi siku 46.
Msigwa amesema hayo yote yamewezekana kutokana kuboreshwa kwa miundombinu katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo uboreshaji huo umerahisisha na kuongeza utendaji kazi kulinganisha na kipindi cha nyuma.


