Na Yohani Gwangway
Mikopo kutoka Taasisi Ndogo za Fedha yaani Microfinance imepaswa kuwa mkombozi kwa wajasiriamali wadogo nchini Tanzania wanaotafuta mitaji ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao na shughuli nyinginezo, ijapokuwa licha ya nia njema ya huduma hizi, wakopaji wengi jijini Mwanza wamejikuta wakitumbukia kwenye tanuru la moto baada ya kukumbana na rungu la uwepo wa riba kubwa ya hadi asilimia 40 kwa mwezi, jambo linalopelekea wengi wao kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kufilisiwa mali zao pamoja na familia zao kuingia kwenye migogoro ikiwemo ndoa kuvunjika.
Katika sehemu ya tatu ya makala hii tunaangalia kwa undani zaidi suluhisho la uhakika ili mikopo hii itimize lengo lake mahususi la kuinua maisha ya Watanzania badala ya kuwazamisha katika dimbwi la matatizo.
Miongoni mwa changamoto kwa wakopaji ni suala la ukosefu wa elimu ya fedha, ambapo wengi wao huchukua mikopobila kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu usimamizi wa fedha. Ni wazi kuwa taasisi za fedha nchini ikiongozwa na Wizara ya Fedha zinatakiwa kutoa mafunzo ya msingi kwa wananchi.
Katika kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi, Benki Kuu ya Tanzania (Bot) imeeleza kuwa imekuwa ikitoa elimu kusuhu masuala ya fedha kwa wananchi.
“Kutoa elimu kwa umma juu ya masuala ya fedha ili kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu maswala ya kifedha ikiwemo maswala yanayohusu viwango vya riba na umuhimu wa kulipa mikopo kwa wakati ili kuepuka ongezeko la gharama na kushindwa kukopesheka siku za mbeleni,” Maelezo ya Benki Kuu ya Tanzania BoT.

Watanzania wengi wameangukia kwenye shimo la madeni kutokana na mikopo na wasifahamu jinsi ya kutoka, hali hiyo inatokana riba kubwa ambazo zimekuwa ni mzigo kwa wakopaji. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uwepo wa riba kubwa huchangiwa na uwepo wa taasisi ambazo hazijasajiliwa, huku baadhi ya taasisi ambazo hazijasajiliwa kuendesha shughuli zao bila kufuata sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa huduma hizo.
“Hili hutokana na uwepo wa watoa huduma ndogo za fedha wanaofanya biashara bila kuwa naofisi, leseni/kibali au kusajiliwa ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa hawaendeshi biashara zao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo iliyowekwa.Vilevile kuwepo kwa watoa huduma wenye leseni ambao hutoa mikopo bila kuzingatiamatakwa ya sheria na Kanuni za usimamizi wa watoa huduma ndogo za fedha ikiwemo Kanuni za kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha,” imefafanua BoT.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine jijini Mwanza, Mwanauchumi Damasi Mushi amesema kuwa wakopaji wengi hukubaliana na riba hizo kubwa kutokana hali ya halisi kiuchumi, yaani ugumu wa maisha.
“Hali ya kiuchumi imekuwa ngumu, kwa hiyo imebidi watu waingie kwenye mitego hiyo ya kuchukua pesa. Mara nyingi mtu akipata pesa ina vishawishi vingi, uwezekano wa kurudisha unakua hauwezekani (mdogo),” maoni ya Mwanauchumi Mushi.
Katika kukabiliana na tatizo hilo la riba kubwa, BoT imetoa elimu kwa taasisi zinazotoa huduma hizo, “Benki Kuu imetoa elimu kwa watoa huduma ndogo za fedha wasiokuwa na leseni kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayosimamia huduma ndogo za fedha juu ya umuhimu wa kupata leseni na madhara ya kutoa huduma pasipo kuzingatia matakwa ya sheria. Elimu hiyo ilitolewa kwa kuzingatia mikoa iliyokuwa na kiwango kikubwa cha watoa huduma ndogo za fedha wasiokuwa na leseni. Mikoa iliyohusishwa katika utoaji wa elimu ni Kigoma, Tabora, Mwanza, Mara, Morogoro, Arusha na Manyara ambapo jumla ya washiriki zaidi ya 600 walipewa elimu” imeeleza BoT.

Kwa mujibu wa Tamko la Sera ya Fedha ya mwaka 2024/25, suala la maamuzi juu ya kiwango cha riba limewekwa mikononi mwa taasisi hizo za mikopo, hali inayopelekea wakopaji kuishia kuwa wahanga wa riba kubwa bila mtetezi.
“Viwango vya riba vitaendelea kuamuliwa na nguvu za soko. Mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba, utaendelea kuchangia katika kuwezesha taasisi za fedha kupanga riba kwa kuzingatia nguvu ya soko. Hivyo basi, riba ya Benki Kuu (CBR), itatumika kama kigezo kimoja wapo katika ukokotoaji wa viwango vya riba,” imeeleza Tamko la Sera ya Fedha la mwaka 2024/25.
Hata hivyobado kuna ulazima wa taasisi za fedha kufanya tathmini ya uwezo wa wakopaji na kuweka riba zinazolingana na mazingira ya uchumi wa kipato cha chini. Aidha, masharti ya mikopo yanapaswa kutazamwa upya ili yawe rafiki kwa wakopaji.
Muda mfupi wa ulipaji wa mikopo kutoka kwenye Taasisi hizi ndogo za fedha pia huathiri uwezo wa wakopaji kufanya biashara zenye faida, ikumbukwe kuwa kutokana na riba kubwa, wajasiriamali hulazimika kujitutumua kulipa mikopo hiyo ndani ya mwezi mmoja, huku wakihofia kuongezeka kwa riba endapo watachelewesha mikopo yao. Hivyo taasisi zinatakiwa kutoa muda wa kutosha unaoendana na mzunguko wa biashara husika ambazo wakopaji wanajihusisha nazo.
Justine Mapunda, mkazi wa Buhongwa jijini Mwanza, akiwa ni miongoni mwa wakopaji ameeleza kuwa wengi wao huishia mikononi mwa taasisi hizo zinazotoza riba kubwa kutokana na uhitaji wa mitaji kwa ajiri ya biashara, pamoja na mahitaji mengine muhimu.
“Kwa sehemu kubwa wengi tunakopa kwa ajili ya mitaji, wengine kuimarisha biashara zao. Ugumu wa maisha, mahitaji ni mengi na hela hakuna, basi mtu unaona ni bora akakope,” amesema Mapunda.
Mapunda ameshauri kuwa mbali na ombi la riba kushushwa kuendana na hali zao za kiuchumi, ni vyema pia muda wa kurejesha mikopo hiyo ukaongezwa ili kutoa nafasi kwa wakopaji kuirejesha kwa wakati.
“Sisi tunavyokopa huwa tunatamani sana angalau muda wa marejesho ya mikopo uongezwe. Wakati mwingine unakopa hela riba kubwa na mtu unatakiwa urudishe ndani ya mwezi, na ukisema uwaombe urejeshe ndani ya miezi miwili ndiyo hivyo riba inazidi kupaa. Hii mikopo ni kichomi,” ameshauri Mapunda.

Wakati riba za taasisi ndogo za fedha ikielezwa kuwa ni mzigo kwa wakopaji walio wengi ikitajwa kuwa asilimia 25 hadi 40, kwa upande wa taasisi nyingine za fedha kama vile benki ambapo baadhi ya benki kama vile NMB zimekuwa zikiingia ubia na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo, mnamo Mei 2024, Benki ya NMB iliingia makubaliano ya miaka miwili na Serikali kwa ajili ya kutoa mikopo yenye riba ya asilimia 7 kwa wafanyabiashara wadogo hapa nchini.
Hata hivyo hii ilikuwa ni bahati ya mtende, kwani Serikali ilitenga kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 18.5, lakini bado wafanyabiashara wadogo pamoja wananchi wa kipato cha chini hushindwa kukizi vigezo ambazo benki husika uhitaji kutoka kwao, jambo linalowafanya kukimbilia kwenye taasisi ndogo za fedha zenye mikopo chechefu inayopatikana kiurahisi.
Wajasiriamali wengi hukopa lakini changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kukosa soko la bidhaa zao. Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini wanatakiwa wawekeze vya kutosha kwenye miundombinu ya masoko, maonyesho ya biashara pamoja na majukwaa ya kidigitali yatakayowaunganisha wazalishaji na wateja.
Vilevile, Serikali pamoja na wadau pia wanatakiwa kuanzisha na kuimarisha bima ya mkopo ambayo itaweza kumlinda mkopaji pale biashara inapokumbwa na changamoto kama vile majanga, ugonjwa au vifo. Kwa kuanzishwa kwa bima ya mikopo, itasaidia kupunguza madhara makubwa kama kufilisiwa mali au migogoro ya kifamilia pindi mkopaji atashindwa kurejesha mikopo hiyo.
Kwa sehemu kubwa baada ya taasisi hizi kutoa mikopo, hujiondoa kwa mkopaji na kunakuwa hakuna ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya mkopaji kwa ajili ya kutoa ushauri wa mara kwa mara pamoja na kutengeneza mazingira rafiki baina ya pande mbili yaani taasisi husika na mkopaji. Hivyo, ufuatiliaji wa maendeleo ya biashara na ushauri wa mara kwa mara ni muhimu kwa mafanikio ya wakopaji.
Mara nyingi mikataba ya mikopo mingi huandikwa kwa lugha tata isiyoeleweka kwa urahisi na wakopaji wa kawaida. Taasisi ndogo za fedha nchini zinatakiwa kuhakikisha mikataba inakuwa ya wazi, rahisina ielezwe kwa lugha anayoielewa mkopaji kabla ya kuingia makubaliano.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imendelea kusisitiza umuhimu wa uelewa juu ya mikataba ambayo wakopaji huingia na taasisi hizo ndogo za fedha. “Benki Kuu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya elimu ya fedha na kutambua haki zao za msingi wanapohitaji huduma za mikopo kutoka wa taasisi za fedha ikiwemo umuhimu wa kupewa mkataba wa mkopo, kusoma na kuelewa kabla ya kukopa,” imesema BoT.
Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inatakiwa izisimamie kwa karibu Taasisi ndogo za fedha nchini kwa kuzijumuisha kwenye mfumo rasmi wa usajili na udhibiti. Katika juhudi za kuondokana tatizo la uwepo wa taasisi ndogo za fedha zisizo na leseni, BoT imekuwa ikiendesha operesheni maalum kuwakamata watoa huduma hizo wasio na leseni.
“Aidha Benki Kuu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imefanya na inaendelea na operesheni maalumu ya kuchunguza, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watoa huduma wasiokuwa na leseni ambao wameendelea kukaidi maagizo. Hadi mwezi Juni 2025 jumla ya watoa huduma zaidi ya 30 wasiokuwa na leseni walifikishwa mahakamani,” imesema BoT.
Ili kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi wa taasisi ndogo za fedha, Mwanauchumi Damasi Mushi amesititiza kuwa mara kwa mara taasisi hizo zinapaswa kupeleka taarifa zao kwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Taasisi hizo zinatakiwa ziripoti shughuli zao wanazozifanya kwa mamlaka husika ambayo ni Benki Kuu, ili hata kama kuna jambo limekaa vibaya, Benki Kuu itakuwa ina uwezo hata wa kuifutia leseni au kusimamia kwa ukaribu zaidi jambo hilo,” amesema Mwanauchumi Mushi.
Ashura ambaye ni miongoni mwa waathirika wa mikopo kutoka taasisi ndogo za fedha, ambapo ndoa yake ilivunjika chanzo kikiwa ni mikopo hii, akiwa na maumivu ya moyoni ametoa neno kwa watu ambao wanataka kukopa katika taasisi hizo.
“Ningependa kuwaambia wenzangu na mimi ambao wanataka kukopa, kabla hujachukua mkopo, hakikisha umeelewa hiyo mikataba yao. Yaani usikubali kusaini kitu ambacho hukielewi kwa kina, maana uelewa mdogo wa mikataba ndiyo umetugharimu wengi,” ameeleza Ashura.
Ashura anatoa rai kwa taasisi zinazotoa mikopo kutanguliza uwazi mbele na kuwahusisha wateja wao ipasavyo hasa kuhusu vipengele muhimu vya mikataba ya mikopo hiyo kabla ya kuisaini.
“Ni wajibu wa taasisi hizi kuhakikisha mikataba yao inaeleweka, isijazwe maneno ya kisheria tu yasiyofahamika kwetu. Pia, watoe elimu kabla ya kutoa pesa ili sisi wateja tufahamu tunachoingia,” amesisitiza Ashura.
Kwa upande wake Amina, ambaye ni mkazi wa Nyang’hingi jijini Mwanza aliyejikuta madirisha yake (aluminium) yaking’olewa kutokana na kushindwa kurejesha mkopo wake amesema taasisi hizi zizingatie suala la ubinadamu pindi pale waposhindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
“Mikopo iwe ni njia ya kujinyanyua kimaisha, isiwe sababu ya kunyanyasa watu. Hata kama mtu ameshindwa kulipa, sio vizuri kumdhalilisha kiasi hicho. Tuonyeshe ubinadamu,” ameshauri Amina.
Ashura ametoa wito kwa Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti kiwango kikubwa cha riba ambacho kimeendelea kuwa mzigo mkubwa kwa wakopaji nchini, kwani wengi wao wamejikuta wakiingia kwenye matatizo kutokana na riba ambayo haiendani na hali halisi ya uchumi wao.
“Sisi bado tunajitafuta kwenye maisha ndiyo maana tunakimbilia mikopo tukiamini kuwa itatusaidia, ila imekuwa kinyume chake. Serikali lazima iingilie kati suala la riba, hatuwezi kuendelea kukopeshwa kwa riba kubwa. Ni mateso,” amesema Ashura kwa uchungu.
Mikopo ya Taasisi Ndogo za Fedha ina nafasi kubwa ya kubadilisha maisha ya watu, hasa kwa jamii ya kipato cha chini nchini Tanzania. Ni jambo lisilopingika kuwa mafanikio hayo hayawezi kufikiwa iwapo mfumo wa utoaji mikopo utaendelea kuwa kinyonyaji na kikwazo badala ya msaada kwa wakopaji. Kwa kuweka kipaumbele kwenye elimu ya fedha, masharti nafuu, usimamizi bora pamoja na kuzingatia utu wa mkopaji, mikopo hii ni safina ya kweli kwa Watanzania kujikwamua kiuchumi.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


