Mapambano dhidi ya uharibifu wa misitu Tanzania: Je, tunashinda au tunashindwa?

Na Dominic Allen

Mazingira ni moyo wa dunia, yakidhoofika maisha ya kila kiumbe huingia hatarini. Ni katika mazingira ndipo tunapopata kila kitu, hewa safi, maji tunayotumia, chakula na hata utulivu wa akili zetu. Katika kila pumzi tunayovuta kuna zawadi itokanayo na mazingira, lakini shughuli za kibinadamu kama vile ukataji wa miti, uchafuzi wa hewa, maji pamoja na matumizi mabaya ya ardhi kumesababisha dosari katika mazingira, na matokeo huonekana kupitia mabadiliko ya tabianchi pamoja na ukame unaoathiri uzalishaji wa chakula.

Leo Juni 05, 2025 ni Siku ya Mazingira Duniani ikiwa na Kauli Mbiu “Komesha Uchafuzi wa Plastiki”, Tanzania imeungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha siku hii. Makala hii inaangazia hali ya uharibifu wa misitu duniani, huku tochi yetu ikiimulika kwa kina zaidi tatizo hili nchini Tanzania, na namna ya kujikwamua tutoke hapa tulipo.

Hali ya uharibifu wa misitu duniani

Misitu inachukua takriban asilimia 31 ya dunia na ni makazi ya zaidi ya asilimia 80 ya aina zote za wanyama, mimea na wadudu wa nchi kavu. Hii inadhihirisha wazi umuhimu wa misitu dunia. Lengo namba 15 la Maendeleo Endelevu linahusu “Maisha ya nchi kavu” likijikita katika kulinda na kurejesha mifumo ikolojia ya nchi kavu, kusimamia misitu kwa njia endelevu, kupambana na kuenea kwa jangwa, kusitisha na kubadili mwelekeo wa uharibifu wa ardhi pamoja na kukomesha upotevu wa bayoanuwai.

Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) katika moja ya chapisho lake lenye kichwa “Simamia misitu kwa njia endelevu, mapambano dhidi ya kuenea kwa jangwa, kusitisha uharibifu wa ardhi na komesha upotevu wa bayoanuwai” lilibainisha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2019, takribani hekta milioni 100 za ardhi yenye rutuba na tija ziliharibiwa kila mwaka ulimwenguni, na kuathiri maisha ya watu bilioni 1.3.

Katika chapisho hilo, shughuli za kilimo zinatajwa kuwa chanzo kikubwa cha ukataji wa misitu duniani, kwani takriban asilimia 90 ya ukataji wa misitu umesababishwa na shughuli za kilimo, ingawa kwa mwaka 2024, moto ndiyo umetajwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa misitu.

Sababu nyingine kuu zinazopelekea uharibifu wa misitu ni pamoja na shughuli za ukataji miti, malisho ya mifugo na ujenzi wa barabara.

Kwa mujibu wa utafiti uliyofanywa Maabara ya GLAD ya Chuo Kuu cha Maryland na kuchapishwa na Taasisi ya World Resources Institute (WRI) umebainisha kuwa hekta milioni 6.7 za misitu ya asili ya tropiki iliharibiwa mwaka 2024, mara mbili ya ilivyokuwa mwaka 2023. Hii ni sawa na takriban viwanja 18 vya mpira wa miguu kupotea kila baada ya dakika 18.

Utafiti huo uliyotolewa Mei, 2025 na kupewa jina la “Moto kuvunja rekodi, upotevu wa misitu ya tropiki, mwaka 2024” ulisema kuwa upotevu huo mkubwa kwa mwaka 2024 pekee ulisababisha uzalishaji wa tani gigatani 3.1 (Gt) za gesi chafu.

Hali ya uharibifu wa misitu Tanzania

Kwa mujibu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), misitu inachukua takriban asilimia 55 ya eneo lote la Tanzania Bara, ambapo jumla ya eneo la misitu ni hekta milioni 48.1.

Katika Mdahalo wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika Kizimkazi mkoa wa Kusini Unguja Agosti 23, 2024, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Christina Mndeme alisema kuwa nchini Tanzania inakadiriwa takriban hekta 400,000 hupotea kila mwaka kwa kukatwa.

Hii ni kutokana na shughuli mbalimbali za ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya kuni, kilimo kisicho endelevu, pamoja na upanuzi wa makazi.

Katika kupambana na uharibifu wa misitu, Tanzania imechukua hatua mbalimbali muhimu, ikiwemo utekelezaji wa Sera ya Misitu ya Taifa ya mwaka 1998 pamoja na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002, ambazo zinalenga kusimamia misitu kwa ushirikiano wa jamii.

Serikali ya Tanzania imeandaa mikakati maalum, ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), wenye lengo la kuimarisha matumizi ya nishati mbadala nchini.

Vilevile Tanzania imeweka mkakati madhubuti wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Misitu kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2031, unaolenga kukuza sekta ya misitu kama nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Dira kuu ya mkakati huu ni kuona sekta ya misitu yenye nguvu inayochangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa huku ikihakikisha rasilimali za misitu zinadumishwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Lengo kuu la mkakati huu ni kusimamia na kuongeza matumizi endelevu ya rasilimali za misitu na miti, ili kuhakikisha usambazaji wa bidhaa na huduma za misitu unakidhi mahitaji ya kitaifa na ya kimataifa. Hii inajumuisha usimamizi bora wa misitu, uimarishaji wa uzalishaji wa bidhaa za misitu, na uhifadhi wa mazingira ili kusaidia maendeleo endelevu.

Kwa kuzingatia malengo haya, Serikali imejizatiti kuimarisha michakato ya usimamizi wa misitu na kuhimiza ushirikiano baina ya wadau mbalimbali, ikiwemo jamii za vijijini, sekta binafsi, na mashirika ya kimataifa. Mkakati huu ni hatua muhimu katika kuendeleza sekta ya misitu kuwa chanzo cha ajira, mapato, na hifadhi ya mazingira nchini Tanzania.

Pia, Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Kimataifa wa REDD+ (Kupunguza Uharibifu wa Misitu na Upotevu wa Misitu), unaolenga kupunguza utoaji wa hewa ukaa kwa kuhifadhi misitu.

Mwezi Mei, 2025 Waziri wa Maliasili na Utalii nchini, Dkt. Pindi Chana wakati akitoa hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026 alisema Serikali ya Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa biashara ya mazao ya misitu na nyuki, jambo linaloonyesha mafanikio ya juhudi za pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi, ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, uzalishaji wa malighafi mbao katika mashamba ya Serikali yaliyolimwa miti kwa ajili ya biashara umeongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka mita za ujazo 1,108,791 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia mita za ujazo 1,264,535 mwaka wa fedha 2024/2025.

“Thamani ya mauzo ya mazao ya misitu nje ya nchi imeongezeka kufikia Tsh. 458,474,543,027.45 mwaka 2024/2025 sawa na asilimia 333.8 ikilinganishwa na Tsh. 105,689,957,500.00 mwaka 2020/2021” alisema Dkt. Chana

Ongezeko hili linaashiria mafanikio katika usimamizi endelevu wa misitu na kuimarika kwa sekta ya mazao ya misitu, ambayo ni chanzo muhimu cha ajira na mapato kwa wananchi wengi. Aidha, biashara ya nyuki nayo imepata mafanikio kutokana na mikakati ya kuhamasisha uzalishaji endelevu na ubora wa bidhaa, jambo ambalo linachangia kuongeza thamani ya mazao ya misitu katika soko la ndani na nje ya nchi.

Ukuaji huu unaonesha wazi namna sekta ya misitu na nyuki ilivyo na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, hasa vijijini ambako shughuli hizi hufanyika kwa wingi. Hata hivyo, mafanikio haya pia yanasisitiza haja ya kuongeza juhudi katika kulinda misitu dhidi ya changamoto kama uvunaji haramu, uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Uendelevu wa mafanikio haya unategemea usimamizi imara, utekelezaji wa sera madhubuti na ushirikishwaji wa jamii katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Wito kwa wananchi, viongozi na wadau

Katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa misitu na mazingira kwa ujumla, wananchi wanapaswa kupewa elimu endelevu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu na madhara ya ukataji miti ovyo.

Viongozi wa serikali, hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa, wanapaswa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na sheria za mazingira pamoja na kuhakikisha kuwa watendaji wa umma wanawajibika ipasavyo.

Aidha, wadau wa mazingira wakiwemo mashirika ya kiraia na sekta binafsi wanatakiwa kushirikiana kwa karibu katika kutoa elimu, kuhamasisha matumizi mbadala ya nishati na kusaidia juhudi za upandaji miti kwa lengo la kurejesha misitu na kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway

Hot this week

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW