Serikali yatoa bure miche ya parachichi kukabiliana na utapiamlo na udumavu

Na Amiri Kilagalila

Serikali ya Tanzania imegawa miche zaidi 3,000 ya parachichi bure kwa wananchi katika wilaya ya Njombe mkoani Njombe, ili kuendeleza jitihada za kukabiliana na udumavu na utapiamlo kwa watoto pamoja na kuinua kipato cha familia katika kaya.

Zoezi la ugawaji wa miche hiyo limefanywa jana Mei 19, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda katika mtaa wa Sido uliyopo Halmashauri ya Mji wa Njombe wilayani humo.

Amebainisha kuwa udumavu wilayani humo bado upo hivyo lazima jitihada ziweze kufanyika ili kupunguza au kuondoa kabisa udumavu kwa kushiriki kampeni mbalimbali ikiwemo ugawaji wa miche ya parachichi.

Sweda ameeleza kuwa wananchi hao wamepatiwa miche hiyo kwa ajili ya kupanda ili baadae waweze kunufaika kwa kupata matunda kwa ajili ya lishe yao pamoja na watoto, na mengine wauze na kupata fedha ili kuinua uchumi wa familia.

“Wakati sisi tunakutengenezea utajiri wa sasa na baadae na familia iwe na lishe bora, nimewaambia miche ya parachichi ni pensheni ukiipanda na kuitinza itakutunza baadae” amesema Sweda.

Sweda ameongeza kuwa zaidi ya walengwa 1,800 wanaotoka kaya maskini watanufaika na miche hiyo huku akiwaomba kutofurahia kuitwa kaya maskini kwa kuitunza miche hiyo ili kubadilisha maisha yao kiuchumi.

Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Juma Sweda akizungumza na wananchi jana Mei 19, 2025 wakati wa zoezi la ugawaji wa miche ya parachichi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 15, 2024 na Wizara ya Afya nchini Tanzania, takribani watoto watatu kati ya kumi wenye umri chini ya miaka mitano hapa nchini wana udumavu kutokana na lishe duni.

Mkoa wa Njombe unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa yenye viwango vya juu vya udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, ukiwa na asilimia 50, hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Machi 01, 2024.

Mwezi Januari, 2025 Mkurugenzi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) nchini Tanzania, Ronald Tran Ba Huy alisisitiza umuhimu wa Sekta ya Kilimo, kuweka ulinzi wa kijamii pamoja na mikakati ya kupunguza utapiamlo kama maeneo muhimu ya kuimarishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tanzania tayari ni kapu la chakula kwa ukanda huu, lakini inaweza kuwa kapu kubwa zaidi. WFP inanunua bidhaa nyingi za ndani kwa ajili ya shughuli zake za kikanda, na hivyo kuna fursa kubwa ya kukuza sekta hii” alisema Ronald wakati akichangia maoni kuhusiana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa upande wake Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Thadeo Luoga hapo jana alisema miche hiyo ya parachichi imetolewa bure kwa wananchi kutokana na agizo la Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alilolitoa mwaka 2022 alipofika mkoani Njombe, ambapo alizitaka Halmashauri zote nchini kuzalisha miche na kuwapatia wananchi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha parachichi.

“Halmashauri ya Mji wa Njombe hadi sasa imezalisha miche 30,140 na miche hiyo tumeshaisambaza katika kata saba na hadi leo tunayo miche 10,000 inazaliwa na Amcos ya Lugenge ambayo nayo tutakwenda kuigawa kwa wakulima” amesema Luoga.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Njombe walioshiriki zoezi la ugawaji wa miche ya parachichi lililofanyika katika mtaa wa Sido, wilayani Njombe.

Mtendaji wa Kata ya Njombe Mjini, Enocy Lupimo amesema licha ya zoezi hilo kwa kushirikiana na Halmashauri katika kupambana na udumavu wamefanikiwa kuzunguka Kata nzima na kugawa mayai kwa watoto chini ya miaka mitano na mama wajawazito.

“Kampeni itakayofuata nimkugawa maziwa kila kaya lita moja na baadae tutafanya Nyama Choma Festival kila mwananchi atakula nyama bure” amesema Lupimo.

Eva Lulandala ambaye ni mkazi wa wilaya ya Njombe amesema miche hiyo ina manufaa makubwa kwao kwani ya kuwaingizia kipato nakukuza uchumi itawasaidia katika lishe za watoto wao na kuondokana na udumavu mkoani humo.

“Tunawashukuru sana kwa kutupa miche hii kwani itatusaidia kupata kipato na lishe kwa watoto wetu kikubwa niwaomba wenzangu tukaitunze” amesema Lulandala.

Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiendeleza juhudi kuondokana na tatizo la utapiamlo na udumavu kwa watoto nchini, Sera ya Afya Tanzania ya mwaka 2007, katika kipengele Na. 5.2.2 inayozungumzia “Uhamasishaji na Ushirikishaji” inasema kuwa bado kuna tatizo la utapiamlo huku kukiwa na ushiriki mdogo wa wananchi katika masuala ya afya.

“Aidha, viwango vya utapiamlo katika jamii viko juu pamoja na ushiriki wa wananchi katika masuala ya afya kuwa ni kiwango cha chini” imeeleza Sera ya Afya ya Tanzania ya mwaka 2007.

Katika kukabiliana tatizo la utapiamlo nchini, Sera ya Afya imesisitiza kufanyika kwa juhudi zaidi za uhamasishaji, ili wananchi waweze kulinda na kudumisha afya bora na endelevu.

Mwandishi: Amiri Kilagalila

Mhariri: Dominic Allen

Hot this week

Mnyonge, mnyongeni ila haki yake mpeni

By Dorlingson Edward Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), leo...

CHADEMA kutoa msimamo wake kuhusu maridhiano

By Veronica Mlyatu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa...

Popular Articles

Safari ya Mashimba katika kutetea jamii ya Wahadzabe

Nchini Tanzania  kuna jumla ya makabila zaidi ya 120...

Polisi waendelea kuwashikilia viongozi wa CHADEMA

Ni siku ya kwanza tangu kukamatwa kwa viongozi wa...

Siku ya Vijana Duniani.

Kwa sasa ni kijana wa miaka 25 ambaye amejiajiri...

BWAWA LA ARBA’AT  LASABABISHA MAAFA NCHINI SUDAN

Watu 30 mashariki mwa Sudan na na wengine 60...

Sand Mining in Tanzania: Trails of Destruction in Lake Victoria and its Environs

By Dominic Allen On November 14th, 2021 in the Geita...

 Utekaji: Fumbo linalotushinda?

Na Yohani Gwangway Taifa la Tanzania kwa miaka mingi limekuwa...

Abduction: Is it a riddle we can’t solve?

By Yohani Gwangway For many years Tanzania has been an...

Mustakabali wa Hewa Safi kwa kila kiumbe

Na Dominic Allen Msingi wa maisha ya viumbe hai yaani...
LAND DWELLERS FACT CHECK HUB VERIFY FACTS STOP MISINFORMATION Trusted Fact-Checking in Tanzania Beyond What You Know VERIFY NOW

Related Articles

Popular Categories

DWELLERS CHECK-HUB Verify Facts. Stop Misinformation Trusted Fact-Checking in Tanzania • Beyond What You Know VERIFY NOW