Na Yohani Gwangway
Rais wa Finland, Alexander Stubb amehitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Tanzania katika kile kinachoonekana kuwa ni kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya mataifa hayo mawili.
Rais Stubb aliambatana na wafanyabishara kutoka nchini Finland ambao walihutubia katika jukwaa la biashara kati ya mataifa hayo mawili lililofanyika Mei 16, 2025. Majadiliano hayo yalijikita katika kuangalia fursa za kiuchumi na kibishara. Mtaalamu wa Uchumi Dr. Bravious Kahyoza ana maoni haya kuhusiana na ziara hiyo.
“Ni ziara muhimu inaimarisha diplomasia ya uchumi ya Tanzania ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiipa kipaumbele”.

Mazungumzo ya Marais hao yaligusia maeneo mbalimbali kama misitu, uwekezaji na Uchumi wa Bluu. Katika eneo la misitu dunia kwa sasa inapambana kumaliza kitisho cha uharibifu wa misitu ya asili ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Nchini Tanzania zaidi ya 55% ya ardhi ni ardhi iliyohifadhiwa ikiwemo misitu, mbuga za wanyama na hifadhi za taifa kwa mujibu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). Kwa upande wa Uchumi wa Bluu Tanzania ina eneo kubwa la bahari pamoja na maziwa ambayo kama yakitumika vizuri yanaweza kubadilisha hali ya kiuchumi.
Katika kuangazia ziara hii hasa katika eneo la uwekezaji, misitu na Uchumi wa Bluu, mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Dr. Bravious Kahyoza anaona maeneo haya yanagusa maisha ya watanzania kwa kuangalia mchango wake katika maisha ya watu.
“Maeneo yote ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania. Sekta kama uchumi wa buluu inachangia zaidi ya USD 9 kwenye ongezeko la thamani ya pato ghafi la nchi na kuajiri zaidi ya watu million 2, huku Sekta ya Misitu ikichangia 4.2% kwenye kipimo hicho cha uchumi na kuajiri zaidi ya watu million 1.7” alifafanua Dr. Kahyoza.
Katika ziara hii ya Stubb, Rais Samia alitaja utayari wa nchi kutumia fursa kwa manufaa ya pande zote mbili. Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa hili linaweza kufanikiwa kama Tanzania itatekeleza ipasavyo sera yake ya mambo ya nje ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2024, Dr. Braviuos Kahyoza anaona Tanzania iko tayari katika ushirikiano huu.
“Tanzania iko tayari kunufaika na fursa hizo kwa sababu imefanyia marekebisho mkakati wake wa Sera ya Mambo ya Nje. Hii ni hatua kubwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,” maoni ya Dr. Kahyoza kuhusu utayari wa Tanzania.
Mpango wa FORLAND (Forestry, Land Use, and Value Chain Development in Tanzania) umeonekana kuwa wa kipaumbele katika ziara ya Rais wa Finland nchini Tanzania. Mpango huu unalenga matumizi ya ardhi na misitu nchini Tanzania ambao ulianza rasmi mwaka 2024 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2028. Katika mpango huu ambao unatekelezwa kati ya Tanzania na Finland malengo makuu ni kuinua njia za kijamii katika kulinda misitu, kuboresha mashamba ya miti na kuongeza thamani ili kusaidia wapandaji wadogo wadogo wa miti, jamii pamoja na wafanyabiashara wadogo.
Tunataka kufahamu kutoka kwa Mtaalamu wa Uchumi, je, ni kwa kiasi gani mpango huu unagusa maisha ya watu.
“Mpango wa FORLAND ni mpango mzuri kwani unafanya wananchi kumiliki ajenda ya uchumi wa mazingira,” alifafanua Dr. Kahyoza.
Kwingineko katika mazungumzo baina ya Marais hawa, Tanzania imetoa wito kwa Finland kushiriki kwenye mkakati wa Nishati Safi kwa Watanzania. Haya yanatokea ikiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa balozi wa ajenda ya nishati safi hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Tanzania inataka kuwa hadi kufikia 2034, asilimia 80 ya wananchi wake wawe wanatumia nishati safi kwa afya zao na kwa mazingira kwa ujumla. Katika kuangazia suala hili Dr. Bravious Kahyoza alikuwa na maoni haya.
“Bila shaka, nishati safi ni muhimu sana kwa ajenda za nchi yetu. Mpango huu utaimarisha sana hatua za Tanzania kulinda mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Dr. Kahyoza.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa Mei 13, 2025, ushirikiano kati ya Tanzania na Finland umedumu kwa zaidi ya miaka 60 ukijikita katika masuala ya elimu, misitu, mageuzi kwenye mfumo wa kodi, usawa wa kijinsia na maeneo mapya ya tabia ya nchi.
Maeneo mengine ya ushirikiano baina ya mataifa haya ni Uchumi wa Bluu, ulinzi, akili mnemba pamoja na Teknoljia ya Habari na Mawasiliano yaani TEHAMA.
Mwandishi: Yohani Gwangway
Mhariri: Dominic Allen


