Na Dominic Allen
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma ametoa wito kwa vilabu vikubwa vya michezo nchini Tanzania kuwa na viwanja vyao vya kudumu, kwani ni jambo la kushangaza kukosa miundombinu hiyo.
Naibu Waziri Mwinjuma ametoa wito huo hapo jana wakati akizungumza kwenye hafla ya Klabu ya Simba kutangaza mkataba wa miaka mitano na kampuni ya JAYRUTTY Investment Company Limited wenye thamani ya Tsh. Bilioni 38, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo amesema kuwa hata Uwanja wa Benjamin Mkapa unaharibika kwa sababu unatumika kila wakati kutokana na shughuli zote kufanyika kwenye uwanja huo.
“Hata uwanja wetu kuharibika kila wakati ni kwa sababu shughuli zetu zote tunataka tufanyie hapo hapo, kwa hiyo tukiweza kuupunguzia mzigo wa matumizi kwa sisi kutengeneza viwanja vya timu zetu hizi angalau ziwe zinafanya shughuli za michezo kule, itafanya tuwe na miundombinu ya michezo ambayo tunaitunza kwa kiwango cha juu kabisa” alisema Mwinjuma.

Katika hafla hiyo JAYRUTTY Investment Company Limited imepewa mkataba rasmi wa kutengeneza na kusambaza jezi na vifaa vyote vyenye nembo ya Klabu ya Simba.
Hata hivyo JAYRUTTY imeahidi kuboresha miundombinu ya Klabu ya Simba, ikiwemo kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 10,000 hadi 12,000.
Naibu Waziri Hamis Mwinjuma amefarijika baada ya kufahamu kuwa moja ya malengo ya JAYRUTTY katika uboreshaji wa miundombinu, ni ujenzi wa uwanja wa kisasa kwa ajili ya klabu hiyo.
“Hili nililosikia leo kutoka kwa mzabuni limenitia moyo sana, hili la kujenga uwanja alilosema mzabuni liwe jambo la kwanza ambalo Klabu ya Simba inatakiwa kufanya” alisisitiza Mwinjuma.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


