Na Dominic Allen
Wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, wametoa taarifa kwa umma wakieleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu kucheleweshwa kwa ripoti za Tume mbili za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambazo ziliundwa kuchunguza masuala ya ardhi yanayolalamikiwa na wakazi wa wilaya hiyo pamoja na kuangalia utekelezaji wa zoezi la uhamaji kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Wananchi hao wanasema kuchelewa kwa ripoti hizo kunazidisha sintofahamu miongoni mwao wanaosubiri majibu kuhusu mustakabali wa makazi yao na matumizi ya ardhi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Katika taarifa iliyotolewa Machi 05, 2026, jamii hiyo imeeleza kuwa tume hizo ziliundwa mwezi Februari 2025, ambapo wameeleza kuwa walitarajia ripoti hizo kutolewa mapema ili kuondoa sintofahamu na kutoa mwongozo wa namna ya kushughulikia changamoto zinazowakabili. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu matokeo ya uchunguzi wa tume hizo.
“Tume zote mbili zilipewa muda wa siku tisini (90) kukamilisha kazi yao na kuwasilisha ripoti kwa umma na serikalini. Muda wa kukamilisha kazi ulitarajiwa kumalizika mwezi Mei 2025, lakini hadi sasa ripoti hizo bado hazijatolewa,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, kuchelewa kwa ripoti hizo kumeongeza hofu kwa sababu masuala mengi waliyopeleka mbele ya tume yanahusu haki za msingi za maisha yao, ikiwa ni pamoja na matumizi ya ardhi, ufugaji na upatikanaji wa huduma za kijamii.Taarifa hiyo ya wananchi wa wilaya ya Ngorongoro, imeeleza kuwa kuundwa kwa tume hizo kulifuatia maandamano ya siku sita yaliyofanyika Agosti 2024 katika Tarafa ya Ngorongoro, ambapo wakazi walieleza malalamiko yao kuhusu sera wanazodai kuwa kandamizi, pamoja na changamoto za huduma za msingi katika eneo hilo.
“Tume hizi ziliundwa kufuatia maandamano makubwa ya siku sita yaliyofanyika kati ya tarehe 18 hadi 23 Agosti 2024 na wakazi wa tarafa ya Ngorongoro (NCA), yaliyoibuka kutokana na malalamiko mbalimbali juu ya sera kandamizi, matumizi ya ardhi na huduma duni kwa wananchi,” imeeleza taarifa hiyo.

Wananchi wameeleza kuwa kuchelewa kwa ripoti hizo kumeongeza hali ya wasiwasi katika jamii, hasa kwa kuwa wengi wao wanahofia kwamba mapendekezo ya tume yanaweza kuathiri maisha yao na shughuli zao za kiuchumi kama ufugaji.Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakazi wengi walishiriki katika kutoa ushuhuda na maoni yao kwa tume hizo wakitarajia kwamba maoni yao yangezingatiwa katika uamuzi wa mwisho.
“Ucheleweshwaji wa ripoti hizi kutolewa kwa umma kumeibua hofu, taharuki na kukatishwa tamaa miongoni mwa wananchi wetu, wanaosubiri kwa hamu ripoti hizo kujumuisha na kutatua masuala ya dharura tuliyowasilisha kwa Tume.”
Miongoni mwa masuala yaliyowasilishwa mbele ya tume hizo ni pamoja na vikwazo katika upatikanaji wa huduma za kijamii, na changamoto zinazohusiana na matumizi ya ardhi na ufugaji.Jamii ya Wamasai pia imeeleza malalamiko dhidi ya Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), wakisema kuwa baadhi ya hatua zinazochukuliwa na mamlaka hiyo zinaathiri maisha ya wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
Wakizungumizia matukio ya kukamatwa kwa mifugo, kutozwa faini na hata kubomolewa kwa nyumba za wananchi, wameeleza kuwa vitendo hivyo vinaongeza hofu kwamba maamuzi yanayohusu mustakabali wa ardhi yao yanaweza kufanywa bila kuwashirikisha kikamilifu.
“Hivi karibuni, maafisa wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamekuwa wakikamata mifugo na kutoza faini, kuvunja nyumba za wananchi na kuzuia mifugo kupata maji, malisho na chumvi,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, wamesema kuna maeneo kadhaa muhimu ya malisho ambayo mifugo yao imezuiwa kuyafikia, hali inayoathiri shughuli zao za ufugaji, ambapo maeneo yaliyotajwa ni pamoja na Ndutu, Ormoti, Embakaai na msitu wa Northern Highland.
“NCAA imekuwa ikizuia mifugo kufika katika maeneo muhimu ya malisho kama Ndutu, Ormoti, Embakaai na Msitu wa Northern Highland.”
Vilevile, moja ya masuala yanayozua mjadala mkubwa ni mpango wa kuwahamisha wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa ya wananchi hao, kuna hofu kwamba uhamishaji huo unaweza kuendelea bila kuzingatiwa kwa maoni ya wananchi, ambapo wametaka uwazi zaidi kuhusu mpango huo pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao.
“Maafisa wa wanyamapori wa NCAA wamekuwa wakitishia wananchi wetu na kuwaambia kwamba maoni ya jamii yalipuuzwa na Tume, na badala yake Tume zimependekeza uhamisho wa wananchi na upangaji wa ardhi ambao utawazuia kabisa wananchi wakazi kufika katika maeneo muhimu ya malisho,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imezungumzia ripoti ya hivi karibuni iliyowasilishwa na Serikali ya Tanzania kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), wakisema kuwa ni ishara kwamba mpango wa uhamishaji unaweza kuendelea.
“Ripoti ya hivi karibuni kuhusu hali ya uhifadhi katika Hifadhi ya Ngorongoro iliyowasilishwa tarehe 1 Februari 2026 kwa UNESCO inaonyesha kwamba serikali inakusudia kuendelea na uhamishaji wa watu nje ya Ngorongoro,” imeeleza taarifa hiyo.
Wananchi wa Ngorongoro wameomba tume hizo kuhakikisha kuwa ripoti zao zinajumuisha ushahidi na maoni yaliyowasilishwa na jamii, wakisisitiza kuwa ni muhimu kwa ripoti hizo kuwa wazi kwa umma ili watu waweze kuona namna tume zilivyozingatia mapendekezo ya mwisho.
Miongoni mwa maombi yao ni kuhakikisha kwamba ushuhuda wote uliotolewa mbele ya tume unawekwa hadharani pamoja na nyaraka nyingine zilizowasilishwa. Aidha, wananchi hao pia wameitaka serikali kusitisha uhamishaji wowote wa wananchi kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, pamoja na kurudisha eneo la wananchi lililomegwa kufanywa pori la Akiba la Pololeti.
“Wananchi wa Ngorongoro na Loliondo hatutakubali uamuzi wowote unaokiuka haki zetu za msingi za kibinadamu,” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa suala la uhamishaji wa watu kutoka katika makazi yao linaweza kuwa na athari kubwa katika haki za binadamu ikiwa halitafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazotambuliwa kimataifa, huku wakibainisha mikataba kadhaa ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, ikiwemo mikataba inayolinda haki za kumiliki mali, haki ya makazi na haki za watu wa asili.
Baadhi ya mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu wa Asili pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Raia na Kisiasa.
Pia wameeleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalinda haki ya kila mtu kumiliki mali na kulindwa mali yake kwa mujibu wa sheria.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 24(1), inaeleza wazi kwamba kila mtu ana haki ya kumiliki mali na ana haki ya ulinzi wa mali yake kwa mujibu wa sheria,” imeeleza taarifa hiyo.
Wananchi wa Ngorongoro wamesema wataendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya suala hilo huku wakisisitiza kuwa wako tayari kutumia njia za kisheria na kidemokrasia kulinda haki zao.
“Tunasimama imara katika azma yetu ya kutumia njia zote halali za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kulinda ardhi zetu, heshima yetu na mustakabali wetu,” imeeleza taarifa.
Kufuatia tuhuma zilizoibuliwa katika taarifa hiyo ya wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro kwamba baadhi ya maafisa wa wanyamapori wamekuwa wakiwatishia wananchi kuwa tume za Rais zilipuuza maoni ya wananchi, na badala yake kupendekeza uhamishaji wa wananchi, pamoja na malalamiko mengine ikiwemo kuzuiwa kwa mifugo kufika katika baadhi ya maeneo muhimu ya malisho, pamoja na uwekezaji wa hoteli kufanyika bila ushirikishwaji wa jamii, Land Dwellers ilimtafuta Kaimu Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Hamis Dambaya, ili kupata ufafanuzi wa mamlaka hiyo kuhusu tuhuma hizo.
Dambaya alisema hakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo, ambapo aliomba atafutwe baadaye. Licha ya jitihada za kumtafuta tena, juhudi zetu ziligonga mwamba, hivyo hatukuweza kupata majibu yake hadi habari hii inachapishwa.
Mjadala kuhusu mustakabali wa matumizi ya ardhi, uhifadhi wa mazingira na haki za wananchi katika Wilaya ya Ngorongoro unaendelea kuwa suala nyeti lenye kuhitaji majadiliano ya kina kati ya serikali, mamlaka za hifadhi pamoja na jamii. Wadau mbalimbali bado wanaendelea kusisitiza umuhimu wa uwazi, ushirikishwaji wa wananchi katika kutafuta suluhisho la kudumu litakalolinda urithi wa kipekee wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, huku likiheshimu haki na maisha ya jamii zinazoishi kwenye maeneo hayo.
Mwandishi: Dominic Allen
Mhariri: Yohani Gwangway


